NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
10 January 2018
WALIMU
wenye madeni halali mkoani Tabora wametakiwa kuhakikisha wanawasilisha
vielelezo vinavyoonyesha uhalali wa madai yao kwa Maofisa Elimu waliopo
karibu nao ili yaweze kufanyiwa kazi mapema.
Kauli
hiyo ilitolewa jana wilayani Igunga na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa
Tabora anayeshughulikia Elimu Suzan Nussu wakati akiongea na walimu wa
Shule ya Sekondari ya Ziba alipokuwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa huo
Aggrey Mwanri ili kukagua ujenzi wa mabweni ya wanafunzi.
Alisema
kuwa ni vema zoezi hilo kilafanyika mapema na kwa makini ili Walimu
wanaodai madai ya haki waweze kupata fedha zao kama alivyoagiza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli hivi
karibuni.
“Nawaomba
walimu wenzangu hakikishe mnawaeleza wenzenu wenye madi kupeleka madai
yao mapema kwa Maofisa Elimu waliokaribu nao ili nao waweze
kuyawasilisha mapema Mkoani kwa ajili ya hatua zaidi…ucheleweshaji
wowote unaweza kuwasababisha walimu wachelewe pia kupata haki yao”
alisisitiza Nussu.
Aidha
Katibu Tawala huyo Msaidizi wa Mkoa aliwaonya walimu na Maofisa Elimu
kutofanya udanganyifu wowote kwani fedha kidogo inaweza ikawasababisha
wapoteze kazi zao na hata kujikuta katika vyombo vya Sheria.
Alisema
kuwa walimu wanapopeleka madai yao ni vema wakajiridhisha kuwa ni kweli
wanadai na madai yao ni kweli ili kujiweka katika mazingira salama.
Nussu
aliongeza kuwa Maofisa Elimu katika Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora
ni vema wakahakikisha walimu wote wanapata taarifa na wanahusika waweze
kufikisha taarifa hizo haraka mkoani.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment