Home » » Kaliua yaonya ufisadi fedha za miradi

Kaliua yaonya ufisadi fedha za miradi


HALMASHAURI ya Wilaya mpya ya Kaliua mkoani Tabora, imetoa onyo kali kwa watumishi wote wa halmashauri hiyo kutokuthubutu kujihusisha na vitendo vya kifisadi katika fedha za miradi ya maendeleo.
Onyo hilo limetolewa juzi na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ibrahim Kifoka, alipokuwa akijibu swali la Tanzania Daima katika kikao cha waandishi wa habari muda mfupi baada ya madiwani wa halmashauri hiyo kumaliza ziara ya siku moja jijini hapa.
Alisema siku zote vitendo vya kifisadi vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya wananchi, hivyo uongozi wa halmashauri hiyo utawachukulia hatua kali watumishi wote watakaobainika kujihusisha na hujuma hizo.
Kifoka ambaye pia ni Diwani wa Silambo, alisema jitihada zilizopo sasa ni kuhakikisha utekelezaji wa miradi na uwekezaji unatekelezwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.
“Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua inaamini kila kiongozi lazima asimamie majukumu yake vizuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Hatutakubali fedha za maendeleo zitumike vibaya, tunataka zitumike vema kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Florence Mwale, ambaye pia ni Ofisa Ardhi na Maliasili, alisema uongozi wa halmashauri hiyo umejizatiti kukabiliana na changamoto za kimaendeleo baina ya wananchi wake.
Alisema rasilimali na fursa za kimaendeleo zilizopo wilayani humo lazima zitumike kwa vitendo kutatua adha mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa