Home » » Diwani anusurika kipigo baada ya kudaiwa kuiba simu

Diwani anusurika kipigo baada ya kudaiwa kuiba simu

KATIKA hali ya kusikitisha, Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Mwisi, Terezia Peter (CHADEMA), juzi amenusurika kipigo kutoka kwa wananchi, baada ya kudaiwa kuiba simu dukani.
Akisimulia mkasa huo, Zawadi Thomas (26), ambaye ni mfanyabiashara wa duka la simu mkazi wa Igunga mjini, alisema Agosti 30, mwaka huu saa 3:00 asubuhi, walikuja wateja watatu, akiwemo diwani huyo.

Alisema baada ya kufika dukani, diwani huyo alimwomba kuangalia simu na ndipo alipompatia simu aina tano tofauti ili achague anayotaka kununua.

Alisema wakati akiendelea kuchagua simu hizo, yeye alitoka nje na kumuacha dukani diwani huyo, akiendelea kuchagua simu na baada ya hapo diwani alitoka nje na kwenda sehemu nyingine.

Alisema baada ya kuondoka diwani huyo, aliingia dukani kwake na alipoangalia simu alizokuwa amempatia diwani huyo achague, alikuta simu moja haipo.

Alianza kumtafuta ili kupata ukweli wa tukio hilo na kumkuta akiwa katika saluni moja.

Alisema baada ya kumkuta walimpekua na ndipo walifanikiwa kumkuta na simu hiyo aina ya Dual Sim Lg 200 yenye thamani ya Sh 35,000, akiwa ameiweka katika nguo zake za ndani.

Baada ya kuulizwa diwani huyo, alikiri kuchukua simu hiyo ambapo alimwomba msamaha na kumlipa Sh 80,000.

Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwayunge, Ally Isike alisema alipokea taarifa hizo kutoka kwa wananchi na baada ya kwenda eneo la tukio alikuta umati mkubwa wa watu ukiwa umefurika katika eneo hilo.

“Kitendo hiki, kimenisikitisha yeye kama kiongozi kufanya hivyo ni kitendo cha aibu, nilipofika pale nilikuta tayari wamekwishamalizana kwa kuomba msamaha na kulipa gharama hiyo, ila kwa kweli kwa kitendo hiki kimenikera sana, viongozi kama hawa hawapaswi kuigwa wala kuongoza watu,” alisema Isike.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa