Na Kulwa Karedia
RAIS Jakaya Kikwete, amemhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Fatuma Kimario kimya kimya.
Habari za kuaminika zilizopatikana jana kutoka Igunga mkoani Tabora na Kisarawe mkoani Pwani, zinasema Kimario amehamishwa wiki mbili zilizopita.
Itakumbukwa siku moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza majina ya wakuu wa wilaya wapya, Kimario aliiambia MTANZANIA kuwa yuko tayari kuacha kazi, baada ya Rais Kikwete kushindwa kumhamisha kituo cha kazi pamoja na kukumbwa na matatizo lukuki wilayani humo.
Alisema angeweza kukataa uteuzi huo, kutokana na kupata vitisho vingi, vikiwemo vya kuandikiwa barua za vitisho, kutumiwa ujumbe mfupi wa simu za mkononi (Sms) na kutukanwa kila anapokwenda kushiriki kazi za ujenzi wa taifa, hasa anapoitisha mikutano ya kujadili kero zinazokabili wananchi.
Alisema kuteuliwa kwake, kulionyesha wazi namna Rais anavyomwamini katika utendaji kazi, lakini si kuendelea kufanya kazi katika Wilaya ya Igunga.
Chanzo hicho, kilisema Kimario amehamishiwa katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, kuchukua nafasi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Elibariki Kingu, ambaye amehamishiwa Igunga.
“Ni kweli ndugu yangu, Rais amemhamisha kimya kimya Mkuu wa Wilaya yetu, Fatuma Kimario kwenda Kisarawe, hii inatokana na DC huyu kutokuwa na uhusiano mzuri na wananchi.
“Amehamishiwa Kisarawe, hapa tumeletewa DC anaitwa Elibariki Kingu kama wiki mbili zilizopita, tunaona ameanza kazi ya kutembelea maeneo mbalimbali kama sehemu ya kujifunza na kutambua mazingira ya Igunga.
“Unajua kuhamishwa kwa Kimario kumetokana na mambo mengi mno, siku zote ambazo amekaa hapa, amekuwa na uhusiano mbaya na wananchi, alishindwa kujitokeza hadharani kutatua kero zao, utakumbuka baada ya tukio lililowahi kutokea katika kijiji cha Isakamaliwa wakati wa uchaguzi mdogo, alipigwa na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alipoteza kabisa mvuto kwa wananchi.
“Kama unakumbuka vizuri lile tukio la Isakamaliwa, lilikuwa ni doa kubwa mno kwake, alipoteza mvuto baada ya kukutwa akiendesha kikao cha siri na watendaji wa vijiji, kata, tarafa na wazee maarufu kwa lengo la kuchafua mkutano wa Chadema.” alisema.
Itakumbukwa katika tukio hilo, alibebwa mzobemzobe na wafuasi wa Chadema, huku watendaji wakiambulia kipigo.
Kimario, alikutwa na gari lenye namba STK 38O6 ambako alitiwa misukosuko mingi hadi kufikia hatua ya kuomba maji ya kunywa.
Itakumbukwa katika tukio hilo, wabunge wawili wa Chadema, Slyvester Kasulumbai (Maswa Mashariki) na Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Kiwanga, walikamatwa na kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, kwa madai ya kumdhalilisha kwa kumvua hijabu kinyume na misingi ya dini ya Kiislamu.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment