Home » » JAPAN YAKABIDHI MSAADA WA MADARASA SITA TABORA

JAPAN YAKABIDHI MSAADA WA MADARASA SITA TABORA

Mwandishi wetu, Tabora
Serikali ya Japan imetoa msaada wa ujenzi wa madarasa tisa katika shule ya sekondari ya Ulyankulu mkoani Tabora, kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya elimu kwa wanafunzi wanaoishi katika makazi ya ulyankulu na wale wanaoishi katika vijiji vya jirani.
Akizungumza katika sherehe maalum ya makabidhiano ya madarasa hayo Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okoda, alisema serikali ya Japan imekuwa ikishirikiana na serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Balozi Okoda, alisema kuwa serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo lengo lake ni kusaidia ustawi wa vijana na kuwawezesha kumudu maisha yao.
Alisema japan imetumia zaidi ya shilingi bilioni tisa katika kusaidia shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na shirika la kuhudumia wakimbizi katika eneo la Kaskazini magharibi ya Tanzania katika kipindi cha miaka mine iliyopita na kusaidia shughuli za kibiashara na uchimbaji wa visima katika eneo la Ulyankulu mkoani Tabora.
Mara baada ya kukabidhi madarasa hayo, mkuu wa mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, aliishukuru serikali ya Japan kwa msaada huo ambao utasaidia maendeleo ya kielimu kwa  vijana wanaoishi katika makazi ya ulyankulu hivi sasa na watanzania kwa ujumla.
Pia aliitumia nafasi hiyo pia kulipongeza shirika la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) kwa kuipa msaada wa gari mbili ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora, ambazo alisema zitasaidia suala zima la utoaji wa huduma mbali mbali katika mkoa huo.
Nao wanafunzi  972 wa shule ya sekondari ya ulyankulu wameushukuru Ubalozi wa Japan nchini kwa kutoa msaada huo ambao walisema wanaahidi kuutumia vizuri ili uweze kuwasaidia wao na vizazi vijavyo.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Ulyankulu Alfred Njire, pamoja na shukrani zake za dhati kwa UNHCR na Serikali ya Japan kwa msaada huo, akatumia nafasi hiyo vilivyo kwa ajili ya kuomba msaada zaidi wa ujenzi wa mabweni, jiko, kuboresha huduma za maji, umeme na  kompyuta kwa ajili ya kusaidia suala zima la utoaji wa elimu katika shule hiyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa