Home » » MADIWANI WATAKA TUME YA UCHUNGUZI

MADIWANI WATAKA TUME YA UCHUNGUZI

na Hastin Liumba, Tabora
MADIWANI wa halmashauri ya Manispaa ya Tabora, wameagiza iundwe tume huru ya kuchunguza madai ya utendaji kazi usioridhisha kwa baadhi ya watendaji wa manispaa hiyo.
Hatua hiyo ilifikiwa kwenye kikao maalumu cha Baraza la madiwani kilichoketi jana, ambacho kilizungumzia hali ya mapato na matumizi ya halmashauri hiyo kuwa hayaridhishi kutokana na miradi inaonesha kuwa fedha zimetumika, lakini haijakamilika.
Walisema, kutokana na hali hiyo, wanamuomba mkuu wa mkoa Fatma Mwasa kuunda tume huru itakayochunguza madai hayo ili hatua zaidi zichukuliwe.
Kwa mujibu wa msemaji wa madiwani wa CCM, Seleman Maganga taarifa zilizofikishwa katika kikao hicho, hazina kitu kipya, hivyo hawatazipokea.
"Tunazikataa taarifa zote ambazo hazina jipya lolote tofauti na agizo letu katika kikao kilichopita hapa inaonyesha maagizo ya madiwani yanakuwa magumu kutekelezwa kitu ambacho sisi hatutakubali," alisema Maganga.
Naye, Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Kulwa Shaban alikiri kuwa, ukusanyaji mapato ya halmashauri hiyo, umekithiri udanganyifu kwa kuwa hata kwenye baadhi ya vitabu vinaandikwa shilingi 50,000, lakini ndani yake unakuta shilingi 10,000.
"Ni dhahiri upo mwanya mkubwa wa ulaji fedha, hatutakubali hali hii iendelee kwa wajanja wachache kutokuwa waadilifu kwenye makusanyo, hatua zichukuliwe." alisema.
Naye msemaji wa kambi ya upinzani toka CHADEMA, Hamis Mlewa aliunga mkono kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya watendaji wabadhirifu kwa kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi.
Naye mkurugenzi wa manispaa Tabora, Hadija Makuwani alisema hoja zote zilizowasilishwa atazifanyia kazi na kuweka kila kitu wazi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa