Home » » JK ATUMA RAMBIRAMBI TABORA

JK ATUMA RAMBIRAMBI TABORA

na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa, kufuatia taarifa za vifo vya watu 17 wakiwemo watoto watano vilivyosababishwa na ajali ya basi la Kampuni ya Sabena, iliyotokea katika eneo la Kitunda, Wilaya ya Sikonge juzi.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema kuwa Rais Kikwete amesikitishwa na kuhuzunishwa na vifo hivyo vya papo hapo kutokana na kukosekana kwa busara na hekima ya madereva na uwajibikaji wa pamoja wa vyombo vyenye dhamana na usimamizi wa sheria ya usalama barabarani.
“Kwa dhati ya moyo wangu, ninakutumia wewe mkuu wa mkoa salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kutokana na msiba huo mkubwa uliotokea mkoani kwako. Aidha naomba unifikishie rambirambi hizi kwa ndugu na jamaa wa watu wote waliofikwa na msiba huu.
“…Nawaomba wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu wa kuomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao. Ninawahakikishia kuwa niko pamoja nao katika maombolezo haya,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake.
Pia alimuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe kupona haraka majeruhi 78 wa ajali hiyo, ili warejee katika hali ya kawaida na kuungana tena na ndugu na jamaa zao.
Wakati huo huo, Rais Kikwete jana aliwasili nchini Ghana kwa ajili ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Prof. John Atta Mills ambaye anazikwa leo.
Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi 16 na wageni wengine wengi maarufu, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, kushiriki mazishi hayo ya yatakayofanyika mjini Accra.
Rais Atta Mills (69), alifariki mchana wa Julai 24 mwaka huu, kwa ugonjwa wa kansa ya koo kwenye hospitali ya kijeshi ya 37 Military ya mjini Accra.
Kwa sasa nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa makamu wake, John Dramani Makama.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa