Home » » OPERESHENI YA DC KINGU YAZAA MATUNDA IGUNGA

OPERESHENI YA DC KINGU YAZAA MATUNDA IGUNGA

Na Abdallah Amiri, Igunga

OPERESHENI maalumu iliyoanzishwa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Elibariki Kingu, imeanza kuzaa matunda, baada ya kumnasa mtuhumiwa wa mauaji Makala Kishiwa ( 35).

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya mauaji ya Mandalu Maduhu (30) ambaye ni mkazi wa Kata ya Nanga wilayani humo Julai 30, mwaka huu.

Operesheni hiyo imefanywa na vikosi maalumu vilivyoundwa na DC Kingu kila kata, pamoja na masuala ya ulinzi, pia vinakabiliana na vitendo vya mauaji ya vikongwe vinavyofanywa na watu wachache kwa malengo yao binafsi.

Kuhusu kikosi hicho, Kingu, alisema kimefanikiwa kumnasa Makala Kishiwa ( 35), ambaye anatuhumiwa kufanya mauaji hayo.

Alisema Maduhu aliuawa saa tatu asubuhi kwa kupigwa fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili akidaiwa kuiba baiskeli ya Mipawa Kabota yenye thamani ya Sh 120,000.

Inadaiwa mtuhumiwa baada ya kufanya mauaji hayo, yeye na wenzake walitoroka na kwenda kujificha katika Wilaya ya Nzega.

Hata hivyo kikosi kazi kilichoundwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wilayani Nzega, walifanikiwa kumnasa mtuhumiwa huyo akiwa katika Baa ya Grand Villa ya mjini Nzega.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Anthon Lutha, amethibitisha kukamatwa kwa Kishiwa na alisema atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa