Home » » AKINA MAMA WATAKIWA KULIOMBEA TAIFA

AKINA MAMA WATAKIWA KULIOMBEA TAIFA

Na Abdallah Amiri, Igunga
MKUU wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, amewataka akina mama kuongeza kasi ya maombi kwa ajili ya kulinusuru Taifa lisiwe na vijana wanaojihusisha na vitendo viovu.

Alikuwa akizungumza mjini hapa jana, wakati wa sherehe za uzinduzi wa Tawi la Akina mama Wanaowasiliana kwa Njia ya Maombi (MOMS), zilizofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Igunga.

Alisema karibu asilimia 80 ya vijana wamekuwa wakijihusisha na matukio maovu, jambo ambalo linahatarisha uhai wa Taifa.

“Baba Paroko napenda kukwambia kwamba, nilipofanya ziara ya kutembelea Gereza la Igunga, nilikuta karibu asilimia 80 ya mahabusu ni vijana, nilishituka, maana unaona namna gani nguvu kazi ya Taifa inavyopotea, lazima tusali na kuomba mno,” alisema Kingu.

Alisema hata kama waumini watafanya maandamano kwa miaka tisa kumuomba Mungu, lakini bila ya kubadilisha tabia itakuwa ni sawa na kazi bure.

Awali, Mwenyekiti Msaidizi wa MOMS, Martha Bayo, alisema historia ya tawi hilo ilianza mwaka 1984, huko Abbotisford British Columbia na mwanzilishi ni mama mwombaji, Fern Nicholas, aliyeleta mafanikio makubwa.

Alisema huduma hiyo imeendelea haraka, kwa kuwa kila inapotajwa huwagusa wasikiaji, hasa akina mama ambao ndio wanaolea watoto.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa