Home » » MAGHALA MATATU YA PAMBA YAUNGUA TENA IGUNGA

MAGHALA MATATU YA PAMBA YAUNGUA TENA IGUNGA

Na Abdallah Amiri, Igunga
MAGHALA matatu ya Kiwanda cha Pamba cha Vearrian Tanzania Ltd, yameungua mjini hapa juzi. Baada ya maghala hayo kuungua, Mkuu wa Wilaya Igunga mkoani Tabora, Elibariki Kingu, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wa kiwanda hicho na kuwahoji na hatimaye kujua chanzo cha moto huo.

Alisema viongozi wa kiwanda hicho lazima wakamatwe na wafikishwe katika vyombo husika waweze kuhojiwa kwa kuwa haiwezekani kiwanda hicho kiwe kinaungua mara kwa mara bila kujua chanzo chake na viongozi kuendelea kukaa kimya.

“Siwezi kukubali kuona kiwanda hicho kikiwaka moto mara kwa mara bila kujua chanzo cha moto huo.

“Hata hivyo inaonyesha kuwa, wamiliki wa kiwanda hicho wamekuwa wakitia shaka kwa majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kusababisha kuchafua mazingira pamoja na kuleta hatari pindi kiwanda kinapokuwa kinaungua,” alisema Kingu.

Kwa upande wake, Ofisa Utawala wa Kiwanda hicho, Suleman Ramadhani, alisema yeye tangu afike kwenye kiwanda hicho ana mwaka mmoja na majanga ya moto yanayotokea ni kwa bahati mbaya.

Alisema hasara iliyotokea katika kiwanda hicho ni kubwa ambapo kilo 2,622,740 za pamba zenye thamani ya Sh bilioni 1.8 iliteketea.

Alisema kwa sasa wanatafuta maghala ya kukodi kwa ajili ya kuhifadhia pamba inayoletwa kiwandani hapo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa