Home » » WATAALAMU WA MAABARA WAPEWA SOMO

WATAALAMU WA MAABARA WAPEWA SOMO

na Moses Mabula, Tabora
WATAALAMU wa maabara za tiba Tanzania (MeLSAT), wametakiwa kutojiingiza katika siasa na badala yake wajikite zaidi katika kazi yao ya kutoa huduma kwa wagonjwa.
Wito huo ulitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwassa, alipokuwa akifungua kongamano la 26 la sayansi na mkutano mkuu wa mwaka wa MeLSAT uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma mjini Tabora.
Alisema mtaalamu wa maabara kujihusisha na siasa ni kutoitendea haki jamii, hivyo akawataka kuacha mara moja tabia hiyo, ili kuongeza ufanisi kazini.
“Huwa inauma sana wanasayansi kujiingiza katika masuala ya siasa, na nilikuwa nasubiri mahala pa kusemea, sasa leo nimepata sehemu hii napenda sana nisisitize jambo hili, achani kabisa kutamani siasa, mtaua watu ninyi ni watu muhimu sana kwa taifa,” alisisitiza Mwassa.
Alitaka kongamano hilo liwe chachu ya kuleta mabadiliko katika sekta ya maabara za tiba hapa nchini na kwamba wataweza kupata fursa ya kubadilishana uzoefu, kuwajengea uwezo zaidi wa kuwahudumia wagonjwa pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili sehemu zao za kazi.
Awali, Rais wa chama hicho, Sabas Mrina, alisema kongamano hilo limelenga zaidi kuimarisha ushirikiano ili kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa jamii wanayoihudumia.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa