Home » » Kaliua yanunua maabara zinazotembea

Kaliua yanunua maabara zinazotembea

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora imenunua maabara zinazotembea kwa kata zote nane zenye thamani ya sh milioni 48.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Ibrahim Kifoka Ibrahim, alisema hayo kwenye mahafali ya saba ya Shule ya Sekondari Uyowa.
Alisema licha ya kununua maabara hizo pia halmashauri imetenga sh milioni 19 toka mapato yake ya ndani kujenga maabara katika Shule ya Sekondari Uyowa.
“Tumejipanga vema katika kusadia eneo la sayansi kwa shule za sekondari na msingi…..kiasi cha sh milioni 48 zimenunua maabara zinazotembea na sh milioni 19 za ujenzi wa awali wa maabara ya sekondari ya Uyowa ni mapato ya ndani,” alisema Ibrahim.
Alisema halmashauri imejipanga kukabiliana na changanoto zote zinazoikabili sekta ya elimu hasa sayansi wilayani Kaliua.
Katika hatua nyingine, makamu mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wazazi na watendaji wa kata kusaidia kuwarejesha watoto waliotoroka shule kwa muda mrefu sasa.
Alisikitishwa na hali ya watoto waliohitimu kidato cha nne ambapo awali walianza wakiwa 132 na waliohitimu walikuwa wanafunzi 52.
Ameagiza watendaji wa kata, vijiji na vitongoji kwa kushirikiana na wazazi wa wanafunzi hao kuwasaka watoto wote waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa