WANAWAKE wawili wilayani Nzega, mkoani Tabora,
wameuawa kwa kukatwa katwa mapanga katika matukio mawili tofauti yaliyotokana
na migogoro ya ardhi na kifamilia.
Tukio la kwanza limetokea katika Kijiji cha Iboja,
Kata ya Sigili ambapo mwanamke mmoja ameuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na
ugomvi wa mashamba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Diwani wa
kata hiyo, Pelle Izengo, alimtaja mwanamke huyo kuwa ni G’wallu Kibunga (55),
mkazi wa kijiji hicho.
Alisema tukio hilo limetokea Septemba 7, mwaka huu,
majira ya saa tatu usiku, ambapo wauaji hao ambao hadi sasa hawajajulikana
waliingia ndani ya nyumba ya mwanamke huyo na kuanza kumshambulia kwa mapanga
na kusababisha kifo chake.
Pelle alisema sababu ya mauaji hayo ni ugomvi wa
mashamba ambapo mwanamke huyo alishinda kesi yake katika Mahakama ya Ardhi
Tabora.
Diwani huyo aliwataka wananchi wa kata hiyo
kutojichukulia sheria mikononi, badala yake wafuate sheria ili kunusuru mauaji
ya aina hiyo.
Katika tukio la pili, mwanamke aliyefahamika kwa
jina la Kundi Msweya (70), mkazi wa Kijiji cha Mbagwa, ameuawa kwa kukatwa
mapanga na watu wasiofahamika kijijini hapo.
Tukio hilo limetokea Septemba 4, mwaka huu, majira
ya saa tano usiku ambapo watu hao walimvamia ndani na kuanza kumshambulia kwa
mapanga hadi kusababisha kifo chake.
Matukio hayo yamethibitishwa na Jeshi la Polisi
huku upelelezi ukiendelea ili kubaini waliohusika na mauaji hayo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment