Home » » DC akabidhi madawati 200 Sikonge

DC akabidhi madawati 200 Sikonge

SERIKALI wilayani Sikonge, Tabora imekabidhi madawati 214 kwa shule za msingi 10 yenye thamani ya sh milioni 13.9.
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Sikonge, Hanifa Selengu, alikabidhi madawati hayo baada ya halmashauri ya wilaya hiyo kuanza jitihada za makusudi kuyatengeneza kwa ajili ya shule zilizoko katika wilaya hiyo.
Wilaya hiyo yenye shule za msingi 87 zenye wanafunzi 32,862, inakabiliwa na upungufu wa madawati 6,008 kati ya 14,477 yanayohitajika.
Akizungumza juzi katika hafla fupi ya kukabidhi madawati  hayo kwa ofisa elimu shule za msingi, mkuu huyo wa wilaya alisema wameazimia kutumia mapato ya ndani kutengeneza madawati ili kumaliza uhaba uliopo.
Alisema mkakati mwingine utakaosaidia kumaliza kero hiyo ni kuwabana wafanyabiashara wanaovuna mbao kuchangia asilimia 50 ya mapato yatokanayo na mazao hayo kwa ajili ya madawati.
“Mpaka sasa tumetengeneza madawati 450, leo hii nakabidhi 214 na yaliyobaki yatakuwa tayari Januari. Tumedhamiria kutengeneza madawati 1,000 kila mwaka ili kumaliza upungufu huo,” alisema.
Alisema wataongeza hamasa kwa wananchi na kamati za shule, ili nao wajitolee kutengeneza madawati kwa ajili ya shule zilizopo katika maeneo yao.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa