Na Hastin Liumba,Igunga.
MGOGORO baina ya wananchi na mtendaji wa kijiji cha Simbo wilaya ya
Igunga mkoani Tabora wa kutosoma mapato na matumizi umezidi kushika
kasi baada ya mtendaji huyo kuzidi kukaidi kusoma hesabu hizo.
Mvutano huo ambao ulikuwa wa siku nyingi umechukua sura mpya baada ya
wananchi wa kijiji hicho kufikia uamuzi wa kutaka kumwandikia barua
waziri mkuu Mizengo Pinda ili aweze kutatua kero hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti wananchi hao
walisema kuwa wamefikia maamuzi hayo ya kumwandikia barua waziri mkuu
kutokana na kero hiyo kuchukua muda mrefu pasipo kutatuliwa na viongozi wa
ngazi husika.
Wananchi hao walisema kuwa Ofisa mtendaji wa kijiji hicho ambaye kwa sasa
amehamishiwa kijiji cha Mwanzugi Stanley Ngassa amekuwa akikaidi maagizo
ya viongozi wa ngazi ya wilaya ya kumtaka arudi kijijini hapo ili
asome mapato na matumizi ya kijiji hicho.
Wananchi hao waliongeza kuwa mtendaji huyo amekaidi agizo la mkuu wa wilaya
pamoja na mkurugenzi mtendaji wa halimashauri ya wilaya ya Igunga ambapo
alimwandikia barua ya kumtaka asome mapato na matumizi ndani ya siku 14
ambapo hadi sasa siku hizo zimekwisha pasipo kutekeleza agizo hilo.
Nae Ofisa mtendaji huyo Stanley Ngassa baada ya kutafutwa na waandishi
wa habari kwa njia ya simu ya mkononi ili kuzungumzia juu ya suala hilo
alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo huku akitoa sababu kuwa ana
mgonjwa Hospitalini.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halimashauri ya wilaya ya Igunga
Rustika Turuka alikiri kumwandikia barua mtendaji huyo ya kumtaka arudi
katika kijiji cha Simbo ili asome mapato na matumizi ndani ya siku 14.
Alisema kuwa baada ya mtendaji huyo kudaiwa kuwa amekula fedha za wananchi
amemwagiza Afisa utumishi kumkagua hesabu zake ili kubaini kiasi cha fedha
alizokula na baada ya hapo alipe na awajibishwe kisheria.
“Ni kweli mtendaji huyo nilimwandikia barua ya kumtaka asome hesabu hizo
ndani ya siku 14 lakini baada ya kuona kuwa pia anadaiwa kula fedha za
wananchi nimemwagiza Afisa utumishi kumkagua hesabu zake za fedha ili
kubaini ni kiasi gani alichokula ili azirejeshe na baadaye hatua za
kisheria zitafuata”.Alisema Turuka.
Home »
» MGOGORO KATI YA MTENDAJI WA KIJIJI NA WANANCHI WAZIDI KUSHIKA KAS
0 comments:
Post a Comment