Home » » Wakulima wa Tumbaku wafutwa uanachama

Wakulima wa Tumbaku wafutwa uanachama

Wakulima Sabini na Saba wa chama cha Msingi cha Ushirika cha Luganjo,Kata ya Usinge, wilaya ya Kaliua, wamefutwa uanachama kwa madai ya kulaza madeni hatua ambayo imelalamikiwa kuwanyima haki ya kupata pembejeo kwa msimu huu wa kilimo.
Wakizungumza kwenye Mkutano wa hadhara kijijini Usinge, wakulima hao wamesema hatua hiyo iliyochukuliwa na Afisa Ushirika wa wilaya ya Kaliua, Happiness Mwangomole ni ya uonevu kwa sababu katika msimu uliopita wa kilimo wamelipa madeni yao kwa kati ya asilimia 58 na asilimia 90.
Wamesema wakulima 77 waliofutwa katika chama cha msingi ni wale ambao wamekuwa wakiilalamikia Serikali ya kijiji kwa kutosimamia kikamilifu Maendeleo ya wananchi na kufichua ubadhirifu unaofanywa na viongozi wa serikali ya kijiji hicho.
Mwenyekiti wa CCM wa kijiji hicho, Clement Bigambana amemwomba Mrajisi wa vyama vya ushirika Dodoma kuingilia kati ili kuwasaidia wakulima hao waliofutwa uanachama ili wakopeshwe pembejeo za kilimo kwa lengo la kuwakwamua kujikwamua kiuchumi, kwani uchumi wao unategemea kilimo cha tumbaku.
Katika mkutano huo, wananchi wa Usinge pia wamelalamikia uongozi wa serikali ya kijiji kushindwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za miradi kutoka Serikali kuu kwa muda wa miaka minne sasa na kushindwa kuwachukulia hatua wananchi wana0shawishi wengine kugoma kuchangia asilimia 20 ya miradi ya maendeleo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa