MKAZI wa Kijiji cha Kapiliula, wilayani Urambo, Magdalena Nsimba,
aliyenusurika kifo baada ya kucharangwa mapanga na mumewe kwa madai ya
kukataa kumpa sh 1,000 ya kununulia pombe, amekataa mumewe huyo
kushitakiwa.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Salumu Kululinda, alisema baada ya
mtuhumiwa kukabidhiwa mikononi mwa polisi na kusota rumande kwa siku 14
aliachiliwa kwa kukosekana kwa ushahidi.
Kululinda alisema kuachiliwa kwa mtuhumiwa kunatokana na kitendo cha
Magdalena kumuonea huruma, hivyo kuamua kumsamehe mumewe.
Alisema mama huyo alieleza kutokana na mazingira ya kijijini kuwa
magumu aliona ni vema akubali kumsamehe mumewe, ingawa amejeruhiwa
vibaya, ili wasaidiane kulea watoto wao.
Awali akisimulia mkasa huo, Magdalena, alisema siku hiyo, saa 2
usiku mumewe, Batholomeo John, aliyezaa naye watoto wanne alimtaka
ampatie sh 1,000, lakini alikataa kwa kuzingatia maisha ya kijijini
na muda.
Alisema kutokana na hali hiyo, mumewe alimkata kwa panga maeneo
mbalimbali mwilini na wananchi kwa ushirikiano na uongozi wa serikali
ya kata walimkamata na kumfikisha katika Kituo cha Polisi Urambo.
Hata hivyo, pamoja na kulalamikia kufanyiwa ukatili huo, Magdalena
alisema hawezi kuachana na mumewe na kwamba hayuko tayari kukubali
afungwe.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa umebaini chanzo cha shauri hilo
kutofikishwa mahakamani ni kutokana na Magdalena kukataa kutoa
ushirikiano kwa vyombo vya dola, akihofia usalama wa maisha yake
kutokana na vitisho vya mumewe.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Grecy Lumanyika, alisema kina mama
wengi wa vijijini wamekuwa wakifanyiwa ukatili, lakini serikali
inapofuatilia wanakataa kutoa ushirikiano.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia tukio hilo, akiwemo Salma Mohamed,
wameshauri elimu itolewe juu ya haki za binadamu kwa kina mama na
wananchi wengine wasiojua.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment