BASI la Kampuni ya Taqwa lenye namba ya usajili T 532 BYJ
lililokuwa likielekea nchini Burundi, limegonga magari mawili na
kusababisha kifo cha dereva wake na kujeruhi baadhi ya abiria na watu
wengine.
Ajali hiyo ilitokea wilayani Nzega, Tabora jana ambapo Kamanda wa
Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Peter Ouma,
alithibitisha kutokea juzi saa 2 usiku kwenye Kijiji cha Miguwa.
Dereva wa basi la Taqwa, Adam Msindo, alifariki dunia katika ajali
hiyo inayodaiwa kusababishwa na uzembe wa dereva huyo wa kutochukua
tahadhari wakati analipita gari aina ya Fusso akiwa mwendo kasi.
Kwa mujibu wa Kamanda Ouma, katika ajali hiyo basi la Taqwa lilikuwa
likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Bujumbura, Burundi.
Basi hilo lililigonga ubavuni Fusso lenye namba ya usajili T 134 ACQ
lililokuwa likiendeshwa na Juma Ramadhan akitokea Simbo wilayani Igunga
kuelekea Tinde, Shinyanga.
Kamanda Ouma ameongeza kuwa kisha basi hilo likagongana uso kwa uso
na gari jingine aina ya Scania lenye namba za usajili T 967 APQ na
tela lake lenye namba T 984 AGK lililokuwa likiendeshwa na Halfan
Hussein
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment