KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Kitunda Gold Mining, iliyopo Wilaya
ya Sikonge mkoani Tabora, imeahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi
katika kupambana na vitendo vya kihalifu kwenye msitu wa Kitunda na
eneo la mgodi huo.
Mkurugenzi wa mgodi huo, Samuel Chitalilo alisema hayo hivi karibuni,
alipozungumza na gazeti hili kuhusiana na mipango mikakati ya
kupambana na uhalifu maeneo hayo na kwingineko.
Alisema suala la usalama kwa raia na mali zao ni jambo muhimu,
linalopaswa kuungwa mkono na jamii yote, na alilipongeza Jeshi la
Polisi wilayani Sikonge na Tabora kwa ujumla kwa kuanzisha operesheni
maalumu ya kupambana na vitendo vya uhalifu.
“Kampuni yangu ya Kitunda Gold Mine itaendelea kushirikiana na Jeshi
la Polisi kuhusu kupambana na uhalifu eneo la pori la Kitunda na maeneo
ya mgodi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Chitalilo ambaye pia ni mbunge wa zamani wa
Buchosa, alisema kampuni yake hiyo inakusudia kuanza kutoa vitambulisho
maalumu kwa wachimbaji wote wa mgodi huo.
Alisema vitambulisho hivyo vitachangia kwa asilimia kubwa kuwatambua
vijana wanaojishughulisha na masuala ya uchimbaji madini eneo hilo,
hivyo kurahisisha pia kuwachukulia hatua pale watakapobainika
kujihusisha na mambo mabaya.
Chanzo;Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment