Home » » Nyalandu: Wanaomiliki silaha za ujangili wazisalimishe

Nyalandu: Wanaomiliki silaha za ujangili wazisalimishe

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
 
Serikali imewataka wanaomiliki silaha zinazotumika katika ujangili kuzisalimisha na kuonya kuwa hakutakuwa na msalie Mtume watakapotiwa mbaroni.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema hayo mjini Tabora juzi alipotembelea ofisi za Pori la Akiba Ugalla, ambako alijionea silaha zilizokamatwa katika Operesheni Tokomeza Ujangili.

“Hawa jamaa wanatumia silaha za kivita kuvamia rasilimali zetu. Lakini wakiona huku tumekaza wanakimbilia barabarani na kuanzakupora wananchi wetu, hatutakubali,” alisema.

Alisema umefika wakati kila Mtanzania kulinda rasilimali za nchi na kuonya kuwa yeyote awe raia wa Tanzania au mgeni lazima atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Tutatumia juhudi na nguvu zetu zote kuhakikisha kuwa tunalinda rasilimali zetu kwa kushirikiana na vyombo vyote vya dola nchini ili kumaliza ujangili nchini”.

Alisema si ujangili wa kuua wanyama pekee unaoathiri nchi, bali hata wafugajji wanaoingiza mifugo katika hifadhi na kuharibu mazingira pia watachukuliwa hatua.

Nyalandu alisema wavamizi wote wa hifadhi za taifa na mapori ya akiba wataondolewa kwa mujibu wa sheria na kuwa hakuna atayeonewa haya wala kuonewa.

‘’Nataka wale wote waliovamia mapori ya akiba na hifadhi za taifa waondoke wenyewe kabla ya sheria haijachukua mkondo wake. Hakuna ruhusa ya kuingiza mifugo wala kuendesha kilimo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa. Tutachukua hatua kwa hili,’’ alisema.

Alisema umefika kwa wafugaji kuwa na kilimo endelevu kinachoweza kuwapatia kipato kikubwa na hata wakaweza kuwekeza katika sekta ya utalii, kwani fursa ni nyingi, hususan katika kipindi, ambacho utalii wa Tanzania unakuwa kwa kasi.

Maofisa wanyampori na misitu walisema wamekuwa wakifanya kazi katika wakati mgumu, kwani wafanyakazi na maaskari ni wachache na hivyo kufanya vita dhidi ya ujangili kuwa kubwa kutokana na eneo la hifadhi kuwa kubwa.

“Mheshimiwa, mbali na wafanyakazi, vilevile vitendea kazi ni vichache, hususan magari kwa ajjili ya kufanya doria. Magari yapo, lakini ni mabovu. Tunaomba yafanyiwe matengenezo kama tukikosa mapya,” walisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa