Home » » KAMPUNI YA MABASI 'NBS' YAJIPANGA KUBORESHA HUDUMA ZA USAFIRI NCHINI‏

KAMPUNI YA MABASI 'NBS' YAJIPANGA KUBORESHA HUDUMA ZA USAFIRI NCHINI‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Na Hastin Liumba, Tabora
 
 
KAMPUNI ya mabasi ya NBS inayotoa huduma za usafiri wa abiria ndani na nje
ya mkoa wa Tabora imedhamiria kuboresha huduma zake kwa kiwango cha juu
katika usafirishaji abiria na mizigo.
 
 
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Mohamed Nassoro
Hamdan maarufu kwa jina la Medi katika mahojiano maalumu na mwandishi wa
gazeti hili ofisini kwake.
 
 
Alisema kampuni hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1985 imekuwa ikitoa huduma za
usafiri wa abiria na mizigo katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa
wa Tabora.
 
 
Katika kudhihirisha ubora wa huduma zinazotolewa na kampuni hiyo ndani na
nje ya mkoa huo, Medi  alibainisha kuwa abiria wamekuwa wakiongezeka siku
hadi siku hali ambayo imewalazimu kuongeza idadi ya mabasi.
 
 
Aidha alisema wamelazimika kupanua wigo wa huduma ya usafiri katika mikoa
mbalimbali hapa nchini kutokana na wingi wa abiria wanaosafiri kwenda
maeneo mbalimbali nje ya mkoa wa Tabora.
 
 
'Tumedhamiria kuboresha huduma zetu kwa kuongeza idadi ya mabasi sambamba
na kutoa huduma bora zaidi ndani ya mabasi yetu ili wananchi waendelee
kupata huduma nzuri wanapokuwa safarini', aliongeza.
 
 
Akizungumzia mikakati ya kampuni hiyo, Medi alisema mbali na kuboresha
huduma za mabasi hayo pia wanakusudia kununua mabasi mapya ya kisasa ili
kwenda na wakati sambamba na kutoa misaada mbalimbali ya kijamii pale
inapohitajika.
 
 
Aidha alisema kuwa wamekusudia kuanzisha huduma mpya ya usafirishaji mizigo
ndani na nje ya mkoa huo ili kuwaondolea wananchi kero ya usafirishaji
mizigo yao, na kwa kuanzia tayari kampuni hiyo imenunua 'truck 10' za
magari ya mizigo kwa gharama ya sh mil.720.
 
 
Ili kupanua wigo wa huduma za kijamii, Kampuni hiyo pia imekusudia
kuanzisha mradi wa kilimo na ufugaji ambapo tayari shamba lenye ukubwa wa
ekari 600 limenunuliwa kwa ajili ya ufugaji nyuki, ng'ombe, kuku na mbuzi,
na trekta 2 zilizogharimu sh mil.80 pia zimenunuliwa.
 
 
Alisema kampuni hiyo kama ilivyo makampuni mengine ya usafirishaji
wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara
hasa katika mkoa wa Tabora na mikoa mingine hali inayochangia kukwama au
kuharibika kwa mabasi hasa kipindi cha mvua, hivyo akaiomba serikali
kuongeza jitihada katika uboreshaji miundombinu hiyo.
 
 
Changamoto nyingine wanazokumbana nazo ni vipuli feki vya magari na ubora
wa mizani ya barabarani ambayo huonyesha vipimo tofauti, katika hili alitoa
wito kwa serikali kupitia kitengo chake cha TBS kudhibiti ubora wa vipuri
vinavyoingizwa na mizani ili kumaliza kero hiyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa