Rashid Chambi akiwa ameshikilia moja ya vikombe ambavyo timu yake ya Chipukizi walinyakua.Picha na Hastin Liumba.
Rashid Chambi wa pili toka kushoto waliokaa mstari wa kwanza akiwa na timu ya Chipukizi,pia mwalimu wake na mchezaji wa zamani wa Timu ya Milambo Didas Kunde wa kwanza toka kushoto walioksimama.Picha na Hastin Liumba.
Na Hastin Liumba, Tabora
TANZANIA bado iko kwenye mapambano
makubwa ili kuhakikisha soka lake linakuwa na kupata utambulisho kwenye medani
ya kimataifa.
Aidha bado kumekuwa na kelele za
kuhakikisha kuanza kwa misingi sahihi ya kuinua soka la vijana wa umri mdogo
lakini bado mambo yamekuwa ni mabaya katika uamuzi kwenye mechi za ligi kubwa
nchini Tanzania.
Rashid
Chambi ni kijana wa umri wa miaka 14 ambaye ni kinda wa timu ya Chipukizi yenye
vijana wa chini ya umri wa miaka 17 inayonolewa na mwanandinga wa zamani na beki wa
timu ya Milambo ya Tabora Didas Kunde.
Chambi
alihojiwa na gazeti hili katika mazoezi ya timu yake ya Chipukizi katika uwanja
wa Chipukizi manispaa Tabora ambapo alielezea ni vipi anaona soka la vijana
lilivyo nchini.
Kijana
huyu licha ya kuonyesha uwezo mkubwa katika mashindano mbalimbali na mechi za
mitaani amekuwa mwiba mkali kwa timu pinzani na kivutio kikubwa kwa mashabiki
wa soka.
Anaanza
kwa kusema endapo serikali,TFF na wadau nchini wasipowekeza kwenye soka la
vijana bado nchi yetu haitapiga hatua kwenye medani ya soka hususani soka la
kimataifa.
Chambi
alisema tutapataje timu bora,wanasoka bora ama timu ya taifa itakayoweza
kushiriki kimataifa bila kuwepo usimamizi mzuri toka ngazi ya chini hasa vijana
kama yeye.
Alisema
hadi sasa licha kushiriki mashindano ya Copa Coca-Cola na kucheza kwa mafanikio
makubwa,anashukuru sana timu yake ya Chipukizi ambayo imemlea vyema toka
amejiounga nayo miaka mitatu iliyopita.
Alisema
kila mtu ana kipaji chake ambacho amepewa na Mungu ili aitumikie jamii
inayomzunguka katika mazingira mbalimbali.
Aidha
aliongeza kipaji hicho hasa kwa vijana kinahitaji kutunzwa na kuendelezwa ili
kiwe na manufaa kwa nchi na aliyekitunza kwani ni kitu alichopewa mwanadamu
kama tunu na mwenyezi Mungu.
Anasema
wapo vijana wadogo wengi ambao wanavipaji vya hali ya juu vya kuitumikia jamii
katika sehemu tofauti,lakini kutokana na mazingira yaliyowazunguka wameshindwa
kuonyesha kuwa wanaweza.
Chambi
anasema soka ni mchezo ambao unahitaji maandalizi ya kutosha hasa katika
kuwaandaa vijana wa umri mdogo lakini bado kumekuwa na ubabaishaji kwenye soka
la vijana hadi sasa.
“Nina
imani kubwa endapo vijana wa umri mdogo wataandaliwa vyema kwa kuzingatia
vipaji walivyonavyo watasaidia sana kwenye mashindano mbalimbali.” aliongeza.
Anasema
ipo mifano mingi ya kujifunza na mingine amekuwa akiisoma kwenye majarida na
Television hasa kwa nchi za Afrika za Libya, Nigeria na nyinginezo ambazo
ziliweza kuwandaa vijana kwa muda mrefu na kufanikiwa kufanya vyema.
Alisema
tatizo kubwa linalosababisha soka la Tanzania ni kutokuwathamini vijana wenye
vipaji na badala yake siku zote kumekuwa na hulka ya kutumia wachezaji
wanaoshabikiwa na mashabiki wao.
Chambi
anasema vipaji vya vijana vinamalizwa kutokana na kutothaminika ama kutumika
jambo ambalo mpaka sasa vijana wenye vipaji wamekuwa wakikata tamaa ya
kuendelezwa.
Aidha
anasema kumekuwa na jambo ambalo limekuwa likimshangaza kwani timu ya taifa
siyo sehemu ya kwenda kujifunza mpira, siopokuwa ngazi ya vilabu ndiko mchezaji
anapaswa ajifunze hasa ikizingatiwa mchezaji atakuwa amepitia mafunzo toka katika
vituo vya vijana wadogo.
Alishauri
serikali, wadau na shirikisho la soka nchini TFF, endapo tunahitaji timu bora
ya taifa ama klabu hatuna budi kusimamia vipaji vya vijana ambao wanaweza
kusaidia kwa siku zijazo.
Alisema
vijana wengi ambao anawaona kwenye ligi kuu ya Vodacom Tanzania kuna vijana
wadogo wanawaangaisha wazee kwenye ligi hiyo kubwa.
Alisema
TFF inapaswa kutembelea mikoani kungalia vipaji vingi vilivyopo kuliko kila
timu ya taifa inapotangazwa tunasikia wachezaji wengi wametoka Simba,Yanga na
Azam tu.
Kukatazwa
michezo mashuleni.
Anasema
tatizo kubwa la soka nchini ni pale miaka kadhaa ya nyuma serikali iliamua kutoa
tamko la kukataza michezo mashuleni.
Alisema
katazo hilo lilichangia kuuaa vipaji vingi vya vijana na kurudisha nyuma juhudi
za vijana wenye matarajio makubwa katika kuendeleza vipaji vyao.
Anasema
kwa kiwango kikubwa sasa baadhi ya wachezaji wengi hawajitambui na tuwe na wivu
kwa wenzetu kule ulaya wanavyokuwa na vyuo vya michezo kwa vijana,wanatunzwa na
wanalipwa fedha nyingi.
Serikali iunge
mkono jitihada za vijana.
Chambi
aliongeza kuwa serikali inapaswa kuunga mkono jitihada za vijana wenye vipaji
ambao wamekuwa wakivionyesha kwenye timu zao hasa mashindano ya Copa Coca-cola.
Alisema
serikali imejiweka kando katika kusaidia timu za vijana, timu za taifa na
mashindano mbalimbali hali ambayo inachangia timu zetu zinashindwa kufanya
vizuri.
Nini kifanyike.
Anasema
ili mchezo wa soka ufanikiwe ni vyema serikali ikasaidia moja kwa moja kama
ilivokuwa zamani na timu za vijana chini ya miaka17 iwe chini ya serikali.
Aidha
alisema wachezaji nao wanapaswa kushauriwa vyema ili waweze kuelewa majukumu
yao nje na ndani ya uwanja tofuuti na sasa wachezaji wengi wamekuwa watovu wa
nidhamu.
Uimarishaji
vituo vya vijana.
Chambi
aliongeza ili kufikiwa malengo na njia sahihi vituo vilivyopo vipatiwe walimu
tofauti na sasa vituo kadhaa havina walimu wa kutosha.
Alisema
uwepo wa walimu ni muhimu sana kwani kutasaidia sana kuwapa mbinu vijana
ikiwemo namna ya kucheza soka lenyewe.
Alisema
tukifanya haya kwa kuwekeza kwa vijana wenye vipaji tutafikia mahali swali
tunalojiuliza kila siku la ‘kwanini Tanzania tunashindwa kufanya vyema kwenye
soka’ halitakuwepo.
Mikakati yake.
Anasema
moja ya mikakati yake ni kuhakikisha kipaji chake kinazidi kuongezeka kwa
kuendelea kujituma zaidi katika mazoezi, nidhamu ndani na nje ya uwanja na
kufuata maelekezo ya mwalimu wake.
Aidha anasema kujiamini, kujituma, nidhamu na ushirikiano mzuri na wenzake vimemfanya aweze kufanya vyema kwenye mchezo wa soka hadi sasa.
Anasema
hali hiyo ya kupenda soka aliendelea nayo hadi alipoanza darasa la kwanza mwaka
2006 akiwa shule ya msingi Isike ya mjini Tabora.
Hata
hivyo anasema licha kupenda mchezo wa soka bado amekuwa akifanya juhudi kubwa
kwenye masomo darasani kwani anaamini kuwa soka la sasa bila elimu ni kazi
bure.
Rashid
Chambi ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Kanyenye
iliyopo manispaa Tabora,alizaliwa mwaka 1999 pia ni mkazi wa Kata ya Mwinyi.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment