Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiwa
wanaendelea kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kudai Katiba ya
wananchi, bado viongozi hao wanasisitiza kwamba kamwe hawatarudi kwenye
Bunge la Malaamu la Katiba kama njia za kistaarabu za kuwaomba warudi
hazitatumika.
Kabla ya kuanza kuzunguka mikoani, Ukawa walianza
kampeni za kudai Katiba inayotokana na maoni ya wananchi kupitia Bunge
Maalumu la Katiba.
Ukawa wanapinga mchakato huo kutekwa na CCM, kwa
madai kuwa wamekuwa wakitumia wingi wao ndani ya Bunge hilo kuchakachua
maoni yaliyotolewa na wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ziara za viongozi hao wa Ukawa mikoani, zina lengo
la kuunganisha nguvu za kudai Katiba ya Wananchi na kuwashirikisha
wananchi kuhusu kinachofanywa bungeni.
Vyama vinavyounda Ukawa ambavyo viongozi wake
wakuu wanazunguka mikoani ni Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa,
Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi
Mosena Nyambambe.
Baadhi ya madai ya Ukawa yanayozungumzwa katika
ziara hizo ni mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba na kutekwa kwa
wanasiasa kutoka chama kilicho na wajumbe wengi ndani ya Bunge Maalumu
la Katiba.
Wakati Ukawa wakiendelea na ratiba zao za
kuzunguka mikoani, Bunge Maalumu la Katiba limesimama kwa muda hadi
mwezi Agosti kupisha Bunge la Bajeti ambalo linaendelea mjini Dodoma.
Wenje awasha moto Mwanza
Mbunge wa Nyamagana kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ezekia Wenje, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya fedha ya Ukawa, anasema kuwa hawatarudi kwenye
Bunge la Katiba kama njia za kistaarabu hazitatumika kuwaomba warudi.
Wenje alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza katika viwanja vya Dampo mkoani humo.
Akishangiliwa na umati huo wa watu, Wenje anasema
Ukawa wataendelea kudai Katiba ya Wananchi hadi pale itakapopatikana.
“Kutokana na mapambano yangu bungeni sasa jina limebadilika. Najulikana
Jenero na siyo mtoto wa mama ntilie tena na kwa kudhihirisha hilo
nitahakikisha maoni ya wananchi hayachakachuliwi na Katiba
itakayopatikana itakuwa ya wananchi wote,” anasema.
“Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) namtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda atumie njia
za kistaarabu na kuonyesha ustaarabu katika kutusihi turudi kwenye
Bunge Maalumu la Katiba mwezi Agosti la sivyo, hatutarejea ng’o,”
anasema
Anasema kama watakwenda kinyume na kutumia njia wanazozitaka wao
ili warudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wao wataendelea na msimamo
wao hadi hapo Katiba ya wananchi itakapopatikana.
Amshukia Kinana
Katika hatua nyingine mbunge huyo wa Nyamagana
amewataka wananchi kuwapuuza viongozi wa CCM wanaopita na kupiga
propaganda kwamba katiba haina faida kwao.
Kuna watu wanapita na kuwadanganya kuwa katiba
haina faida kwenu kwa kuwa haiwezi kuwaletea chakula. Hizo ni propaganda
zipuuzeni, anasema.
Anasema anashangaa kusikia kwamba Katiba haiwezi
kuwasaidia wananchi kupata chakula, kwani huo ni uzushi wa kisiasa na
kwamba Watanzania wasisikilize maneno ya wanasiasa hao.
Wenje anaeleza kuwa Watanzania wa leo siyo kama wa
miaka iliyopita, kwani wengi wao wamesoma na wanajua mambo hivyo huwezi
kuwadanganya kwa propaganda za kisiasa.
Mchakato ulivurugikia Ikulu
Wenje anasema “Naomba niwaambie ndugu zangu wa
Mwanza, kwamba mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, ulivurugwa tangu hatua
za uteuzi wa wajumbe wa kundi la wajumbe 201 waliyoteuliwa na Rais
Jakaya Kikwete, kwani idadi hiyo ni kubwa na imejaa makada wa CCM.”
Anaendelea “Kazi inayofanywa na baadhi ya wajumbe
walioteuliwa na Rais Kikwete ni kutetea mambo wanayotaka CCM, jambo
ambalo siyo jema, kwani Katiba siyo ya CCM ni mali ya Watanzania wote.”
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment