Home » » TABORA "WAMKAANGA" KAPUYA ,DC KWA KATIBU MKUU CCM

TABORA "WAMKAANGA" KAPUYA ,DC KWA KATIBU MKUU CCM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Kaliua. Kundi la wanachama wa CCM wilayani hapa limemshtaki Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa amekuwa kinara wa kuweka makundi yanayopigana vita wilayani hapa.
Wakati kundi hilo likitoa tuhuma hizo, kundi jingine limemtuhumu Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Exavery Maketa kuwa amekuwa akiongoza wilaya hiyo kibabe na hataki kushirikiana na wanachama wa chama hicho.
Malumbano hayo yalitaka kuvuruga amani jana katika kikao cha wajumbe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora katika kikao chao na Kinana aliye ziarani mkoani humo.
Kinana baada ya kupokea taarifa ya wilaya hiyo pamoja na ile ya CCM aliruhusu wajumbe hao kuuliza maswali.
Mmoja wa wanachama, Gabriel Mkuya alisema, “Mbunge wetu Kapuya ni kinara wa makundi katika wilaya hii kwani amekuwa akisababisha wanachama wachukiane badala ya kuwaunganisha ili kukijenga chama.”
Naye Mwenyekiti wa Wazazi wa wilaya, Hassan Kataga yeye alimtuhumu mkuu wa wilaya.
hiyo, Maketa kuwa aliendesha operesheni ya kuwaondoa wananchi katika Kijiji cha Bomabuhenga walikokuwa wamejenga jirani na hifadhi ya misitu.
“Mkuu huyu wa wilaya ni mbabe, atasababisha chama kikose kura katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu amekuwa akiwabughudhi wanavijiji, tunaomba ahamishiwe wilaya nyingine,” alisema huku akishangiliwa na kundi jingine linalomuunga mkono Profesa Kapuya.
Kataga alisema mkuu wa wilaya amekuwa akiwaweka sero watu wanaokwenda kinyume na matakwa yao.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Maketa alisema tuhuma hizo hazina ukweli wowote bali zinatungwa na watu wasiopenda usimamizi wake wa sheria na kanuni katika wilaya hiyo.
Akizungumza na wajumbe hao, Kinana alisema: “Nimegundua hapa kuna mgawanyiko mkubwa, mmeonyesha kuwa nyie si wamoja.”
Alisema hawezi kusuluhisha suala hilo haraka bali atatuma ujumbe kutoka Makao Makuu ya CCM kwenda katika wilaya hiyo kuzungumza na makundi hayo ili kupata suluhu.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa