Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUNGE wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage, anadaiwa kuwasaliti
wabunge wa mkoa wa Tabora kwa kupeleka taarifa kwa waziri mkuu Mizengo
Pinda, juu ya mipango ya wabunge wa mkoa huo kuishinikiza serikali ya
Chama cha Mapinduzi (CCM)kutekeleza miradi ya maendeleo ya mkoa.
Rage alidaiwa kufanya usaliti huo Katika bunge la bajeti la mwaka
jana wakati wabunge wa mkoa wa Tabora walipokaa kwa pamoja na kutaka
kususia bajeti ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kutokana na
kuendelea kusuasua kwa miradi ya maendeleo ya mkoa huo hususan miradi ya
barabara.
Chanzo kutoka kwa mmoja wa wabunge wa mkoa huo, kilieleza lengo la
wabunge hao ilikuwa ni kutoka nje wakati wa kusomwa kwa bajeti ya wizara
ya ujenzi 2013/2014, ili kuonyesha namna serikali ya CCM ilivyoshindwa
kuthamini uzalendo wa wananchi wa mkoa wa Tabora
“Tulikaa kwa pamoja tukajiuliza kosa letu Tabora ni kuwa na majimbo
yote yanayoongozwa na CCM ama unyonge wetu wa kushindwa kupigania
maslahi ya wananchi kwa ajili ya kukilinda chama..tukasema hapana lazima
sasa tuonyeshe kukerwa kwetu na njia nzuri tulichagua kususia bajeti ya
Wizara ya Ujenzi,” kilieleza chanzo chetu.
Alisema muda mfupi kabla ya bajeti ya wizara hiyo haijasomwa, wabunge
wa Tabora wanaotokana na CCM waliitwa katika kikao cha dharura kwa
kupigiwa simu na Waziri Mkuu Pinda, kwa ajili ya kutafuta muafaka.
Alisema katika kikao hicho ndipo walipobaini Waziri Mkuu alifikishiwa
taarifa na Rage, hali iliyomfanya mmoja wa wabunge wa viti maalum
kuangusha kilio.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba,
alikiri kukutana na Waziri Mkuu pamoja na Naibu Waziri wa Uchukuzi kwa
wakati huo na kusema kuwa kikao hicho hakikuitishwa na Waziri Mkuu huku
akikanusha mpango wa wabunge kutaka kususia bajeti ya Wizara ya Ujenzi
Alisema baada ya kikao hicho baadhi ya mambo yalishughulilikiwa na
kwamba katika bajeti ya mwaka huu barabara ya Sikonge-Mpanda imetengewa
fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake
Kwa upande wake Rage alipoulizwa alikana mwaka jana wabunge wa mkoa
huo hawakukaa kikao chochote na Waziri Mkuu kwa ajili ya kujadili
kusuasua kwa maendeleo ya mkoa wa Tabora.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment