Home » » JK ALEGEZA KAMBA MASHINE ZA EFDS

JK ALEGEZA KAMBA MASHINE ZA EFDS

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

RAIS Jakaya Kikwete, amewashauri mawakala wanaouza mashine za risiti za kielektroniki (EFDs) kuwaongezea muda wafanyabiashara wa kulipa gharama za mashine hizo ili kuondoa malalamiko ya gharama kubwa za mashine hizo.

Aidha,Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemshukuru Rais Kikwete kwa kuwasaidia kuhamasisha matumizi ya mashine hizo.

Akiwa katika siku ya pili ya kutembelea Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa yaliyofikia kilele chake jana katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Rais alipongeza kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo.

Akiwa kwa mawakala wanaouza mashine hizo za EFds, Rais alisema kutokana na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu gharama za mashine hizo ni vema kuwaongezea muda wa kulipa.

"Kama ni suala la bei kubwa, wapeni muda mrefu wa kulipia mashine hizo na kama wataendelea kulalamika huyo atakuwa na lake,"alisema Rais.

Akiwa katika banda hilo la TRA, alipokewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Rishad Bade ambaye alimweleza kazi wanazofanya ikiwemo uanzishaji wa mifumo miwili mipya ya usafirishaji mizigo nje ya nchi.

Bade alisema, mfumo huo wa forodha uliounganishwa na TANCIS utasaidia katika kudhibiti upotevu wa mizigo na nyaraka mbalimbali katika nchi za Jumui ya Afrika Mashariki.

Akiwa katika banda hilo,Rais Kikwete alifurahia uanzishwaji wa vilabu mbalimbali vya kodi katika shule za sekondari kwa nia ya kuwajengea vijana moyo wa kulipa kodi.

Mara baada ya ziara ya Rais, Bade alimshukuru Rais kwa kuhamasisha jamii kutumia mashine za EFDs jambo lililofanya suala hilo kuwa rahisi na wananchi kuitikia kwa nguvu.

Alisema, katika maonesho hayo TRA wameshika nafasi ya pili kwa taasisi za serikali huku akiweka bayana kuwa mifumo mipya miwili waliyoanza kutumia Julai Mosi, mwaka huu itarahisisha ufanisi katika huduma zao za ukusanyaji mapato.

Katika ziara hiyo, Rais Kikwete alianza kwa kutembelea Banda la Mamlaka ya Elimu ya Ufundi (VETA) ambapo alifurahia ugunduzi wa bidhaa mbalimbali na kutaka ubunifu huo kuendelea zaidi.

Alipofika katika kitanda kilichotengenezwa kwa mchanganyiko wa mbao za msufi na nyinginezo aliwataka kutumia miti hiyo iliyoko mingi katika maeneo mbalimbali nchini.

Rais Kikwete pia alitembelea mabanda mengineya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),Kampuni ya Simu (TTCL)Shirika la Hifadhi za Jamii la PPF,Chuo Kikuu cha Ardhi,Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika mabanda hayo alipongeza juhudi wanazofanya za utoaji huduma na kutaka kuongeza uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuongeza ubunifu katika huduma zao.

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa