MAJINA ya abiria
waliofariki na kujeruhiwa katika ajali mbaya iliyohusisha mabasi mawili
ya AM Coach namba T 803 AGN aina ya Scania na Sabena namba T 110 ARV
aina ya Scania, katika Kijiji cha Mlogola, Wilaya ya Sikonge, mkoani
Tabora yametambuliwa.
Katika ajali hiyo
ambayo imetokea Agosti 19 mwaka huu, basi la AM lilikuwa likitokea
jijini Mwanza kwenda Mpanda na Sabena likitokea mkoani Mbeya kwenda
Tabora ambayo yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu 16,
majeruhi 81.
Kamanda wa Polisi
mkoani humo, Suzani Kaganda alisema kati ya abiria 16 waliofariki, maiti
za watu 13 zimetambuliwa na ndugu zao lakini miili ya abiria watatu
bado haijatambuliwa na imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Kitete.
Aliwataja waliokufa
kuwa ni Patrick Fumbuka, mkazi wa Mbeya, Fred Alex, Emmanuel Madochi
Senga na Mabaga Benedicto Peter waliokuwa wanatokea mkoani Mbeya.
Wengine ni Nicholaus
James, mkazi wa Geita, Aristideth Shirima ambaye ni dereva wa basi la AM
na James Komba ambaye ni dereva wa basi la Sabena aliyekatwa kichwa na
bati.
Wengine ni Jackline
Gregin Lumendika, Nasma Zenda mwenye umri kati ya miaka 6-7, na mtoto
mdogo wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja.
Waliofariki katika
ajali hiyo, 10 ni wanaume, wanawake wanne pamoja na watoto wawili mmoja
wa kiume, mwingine ni wa kike ambapo chanzo cha ajali ni mwendo kasi.
Kamanda Kaganda alisema
katika basi la Sabena kulikuwa na wanafunzi waliokuwa wanakwenda
kufanya mitihani katika Chuo cha Kilimo Tumbi, kilichopo mkoani humo
wakitokea Mikoa ya Mbeya na Iringa ambao ni Anna Kalimo kutoka Iringa na
Joyce Mgeni kutoka Mbeya.
Kaimu Mganga Mkuu wa
Wilaya ya Sikonge, John Buswelu, alisema majeruhi 63 wameruhusiwa na
wengine watatu hali zao bado mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Mkoa kwa
matibabu zaidi.
"Majeruhi wengi
walioruhusiwa walikuwa na majeraha madogo madogo na michubuko katika
maeneo mbalimbali ya miili yao, wanaendelea kutumia dawa wakiwa nyumbani
kwao," alisema.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Deus
Kitapondya, alisema hadi jana walikuwa wamepokea majeruhi 18 ambao
walishindikana kutibiwa katika Hospitali ya Sikonge.
Majeruhi hao ni Meena
Shilindye, Silvesta John, Nyorobi Masaga, Salum Hamisi, Athumani Jafari,
Samweli Asubisye, Mgeta aliyekuwa akienda mkoani Mwanza, Josephat Weya,
Paulo Nyanda, Amosi Dominick, Sgt. Joseph Msumari na Scola Kadati.
Wengine ni Jenifa
Sanga, Tora Mbilinyi, Sikujua Saimon na mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka
moja ambaye mzazi wake wamefariki katika ajali hiyo pamoja na majeruhi
ambaye hawezi kuzungumza na jina lake halijaweza kufahamika mara moja.
Aliongeza kuwa, jeshi
hilo linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo na ukikamilika, wote ambao
watabainika kuwa na makosa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za
kisheria.
Alitoa pole kwa familia ambazo zimewapoteza ndugu zao kwenyeajali hiyo na kuwaombea majeruhi wote wapone haraka.
Salamu za JK kwa RC
Katika hatua nyingine,
Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa huo,
Bi. Fatma Mwasa kutokana na ajali hiyo akisema ameshtushwa, kusikitishwa
na ajali hiyo ambayo imegharimu maisha ya watu na kujeruhi wengine.
"Pokea salamu zangu za
rambirambi kutokana na ajali hii, kupitia kwako, naomba unifikishie
salamu za rambirambi na pole kwa wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na
wapendwa wao..namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema azipokee na
kuzilaza roho za marehemu wote mahala pema peponi," alisema Rais
Kikwete.
Rais Kikwete amewaomba
wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu ambao ni
mgumu sana kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.
Alisisitiza umakini na
usimamizi mzuri wa Sheria za Usalama Barabarani kutoka kwa mamlaka
zinazohusika ili maisha ya wananchi wasio na hatia yasiendelee kupotea
na kusababisha simanzi kwa familia, kupotea kwa nguvukazi muhimu ya
Taifa.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment