Home » » HELSB YAANZA KUPELEKA FEDHA ZA MASOMO KWA VITENDO VYUONI

HELSB YAANZA KUPELEKA FEDHA ZA MASOMO KWA VITENDO VYUONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Dk Shukuru Kawambwa.
 
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) imeanza kutoa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa baadhi ya vyuo ambavyo havikupatiwa fedha hizo.
Fedha hizo zilianza kutolewa kuanzia Jumamosi iliyopita kwenye vyuo vitatu ambavyo ni Chuo Kikuu cha Jordani (Morogoro), Saut (Mwanza) pamoja na Saut (Tabora).

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Musa Mdede, alisema fedha hizo zimeanza kupelekwa katika vyuo vitatu na vingine bado.

Mdede alisema vyuo ambavyo bado havijapewa fedha, ni Tumaini Makumira- Iringa, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMUCCO) na Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Bugando (Mwanza).

Hata hivyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisoba, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, hakupatikana.

Alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu (sms) hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
HELSB ilisema Jumanne iliyopita kuwa fedha hizo zingeanza kupelakwa katika vyuo hivyo kuanzia wiki hii.

Mwaisoba alisema kuwa bodi ilikuwa imeshaandaa hundi hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo  hivyo wanaodai Sh. bilioni 6.6 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.

Kabla ya HELSB kuanza mchakato huo, yalizuka malumbano kati yake na Tahliso ambao walitishia kuandamana kushinikiza kulipwa kwa fedha hizo.

Mwaisoba alisema wanafunzi wa vyuo hivyo walichelewa kulipwa kutokana na fedha kuchelewa kupatikana.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa