MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa taifa liko kwenye mkwamo mkubwa wa kukosa uongozi imara kutokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa, hivyo amewaomba Watanzania waunge mkono vyama vinavyounda Umoja wa Kitiba ya Wananchi (UKAWA) ili viwakwamue.
Alisema kuwa moja ya sekta nyeti ambazo watawala waliyoko madarakani wameshindwa kuziboresha ni elimu, jambo linalosababisha taifa kuzalisha matabaka makubwa katika eneo hilo huku viongozi wakichukulia suala hilo kama jambo la kawaida.
Mbowe aliyasema hayo juzi akiwa katika siku yake ya mwisho mkoani Tabora baada ya kufanya mikutano 36 ndani ya siku nne, ambapo akiwa mjini Sikonge alisema kuwa kupitia ziara yake katika vijiji na miji ya mkoa huo, amezidi kujionea Watanzania wanavyohitaji mabadiliko ya mfumo na utawala.
“Nimepita maeneo ya vijiji na miji mbalimbali ya mkoa wa Tabora, nimejionea kwa macho yangu hali inayowakabili wakulima wa pamba, tumbaku, mpunga na mazao mengine kwa ujumla, nimeona hali inayowakabili wafugaji, jinsi wanavyopitia kwenye mateso ya kunyanyaswa pamoja na mifugo yao.
“Wakulima na wafugaji ni moja ya makundi ambayo kwa sasa yanaweza kuwa mfano mkubwa wa namna ambavyo watawala wa CCM wameshindwa, sera zao zimeshindwa, hawana mikakati tena ya kuwasaidia na kuwainua wananchi wa vijijini ni dalili ya nchi kukwama,” alisema.
Mbowe ambaye juzi aliingia mkoani Katavi kuendelea na ziara itakayokwenda katika mikoa sita, alisema kuwa; “ukitaka kuua taifa lolote duniani ua elimu ya taifa husika; viongozi wetu wameua taifa hili kwa kuharibu elimu yetu”.
“Sasa kama taifa tumekwama kabisa. Tumaini pekee la Watanzania kwa sasa ni kupitia vyama vinavyounda UKAWA na lazima tuanze kupitia kwenye uchaguzi huu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji,” alisema Mbowe.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment