Home » » 30,170 KUWEZESHWA NA MRADI KIELIMU, KIUCHUMI

30,170 KUWEZESHWA NA MRADI KIELIMU, KIUCHUMI

WAKAZI wapatao 30,170 kutoka katika familia maskini katika vijiji 20 vya wilaya za Sikonge, Urambo na Kaliua, mkoani Tabora wanatarajiwa kunufaika kielimu na kiuchumi kutokana na jitihada  za uwezeshwaji zinazofanywa na mradi wa Prosper mkoani hapa.
Mradi huo unaofadhiriwa na Shirika la Elimination of Child Labour Foundation (ECLT) lenye makao yake makuu jijini Geneva, Uswisi umedhamiria kuziinua familia maskini zinazoishi katika vijiji 20 vya wilaya hizo, ili kupunguza umaskini na kuongeza kipato katika ngazi ya kaya.
Hayo yalibainishwa na Waratibu wa mradi huo, Jesca Kibiki wa Sikonge na Paul Medeye wa Urambo katika mikutano miwili tofauti ya kampeni za kutokomeza ajira mbaya kwa watoto.
Walisema mradi huo umedhamiria kuwawezesha kiuchumi vijana wa kiume na kike na kinamama wajasiriamali kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo kilimo bora, ufugaji na ujasiriamali sambamba na kuwapatia mikopo yenye riba nafuu.
Katika mkakati huo, walisema watoto wadogo na vijana wapatao 7,800 wenye umri kati ya miaka 5-17 katika vijiji hivyo 20 wanakusudiwa kunufaika na miradi hiyo ya uwezeshaji ambayo imelenga kuwasaidia vifaa vya elimu wanafunzi wapatao 1800 walioshindwa kwenda shule kwa sababu ya utumikishwaji katika kilimo cha tumbaku na kuwapa malezi na shughuli baada ya masomo vijana 2800 waliokosa elimu.
Walisema mikakati mingine ni kuwapa mafunzo ya ufundi stadi/kilimo bora vijana wapatao 1600 na kutoa mafunzo ya usalama na afya mahala pa kazi kwa wanakijiji wapatao 1600 wanaojishughulisha na kilimo cha tumbaku.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa