MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Tabora Mjini, Moshi Nkonkota, amekanusha malalamiko yaliyotolewa na Mbunge Ismail Rage, kuwa ana mgombea kwenye mkoba aliyemuandaa kuwania jimbo hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini hapa, Moshi alisema amekuwa akichafuliwa kuwa amenunuliwa na mfanyabiashara Emmanuel Mwakasaka ili ambebe kwenye kura za maoni katika kuwania ubunge Tabora Mjini.
Nkonkota, alidai kuwa Mwakasaka siyo mfanyabiashara hivyo hapo Rage hakusema ukweli, bali ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Tabora mjini.
Alisema Mwakasaka yupo kwa ajili ya kukiongoza Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi alizopewa na wanachama na anawajibu wa kukisaidia na si vinginevyo.
Aidha, Nkonkota alisema kwa nafasi zake anawajibika kufanya kazi za chama chake na kukijenga bila kumdhania kuwa anahitaji madaraka yoyote ya udiwani au ubunge, na kwamba hizo ni hisia za wale wanaopenda
kugombea ngazi za juu na kutaka madaraka.
“Mimi ni Mwenyekiti wa chama Wilaya ya Tabora Mjini, natambua kuwa
Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini ni Ismail Aden Rage…kwa sasa ni mbunge wangu anaetekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” alisema Nkonkota.
Alibainisha kuwa, yeye kama mwenyekiti yupo kwa ajili ya kuisimamia serikali ili kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo na siyo vinginevyo.
Alisema chama chochote cha siasa kinategemea kujiendesha kupitia michango ya wanachama na ruzuku, lakini inapotokea mwanachama anajitolea kusadia kwa ajili ya wananchi kwenye maendeleo anapigwa vita eti anataka ubunge ama udiwani.
Alisema kwa siasa za sasa, mambo kama hayo hayatakiwi bali wanachama wa CCM wanatakiwa kujitoa kwa ajili ya chama chao kuliko kukaa na kuchafuana kila kukicha.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment