Home » » RC AONYA JUU YA NGONO ZEMBE

RC AONYA JUU YA NGONO ZEMBE

MKUU wa Mkoa wa Tabora Ludovick Mwananzila wamewataka wananchi kutoendekeza ngono zembe hali itakayosababisha kuongezeka kwa maambukizi mapya ya Ukimwi mkoani hapa.
Alisema licha ya kupungua kwa kasi ya maambukizi hayo katika mkoa huo, iwapo wananchi hawatachukua hatua za kuzuia maambukizi mapya hali itajirudia na kuwa mbaya zaidi ya miaka minne iliyopita.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akiwahutubia wananchi wa wilaya ya Kaliua katika kilele cha Siku ya Ukimwi Dunia iliyofanyika Uwanja wa Michezo wa Kaliua mkoani Tabora.
Mwananzila alisema kwamba juhudi hizo zinapaswa kufanywa na wananchi wenyewe ili kuweza kupunguza maambukizi hayo na si serikali ambayo imekuwa ndio inabeba lawama kwa kila jambo.
“Wananchi fanyeni jitihada za kuhakikisha mnatumia kinga wakati wa kujamiana na si kutumia ngono zembe, hilo ni kosa kubwa sana katika maisha yenu hasa katika kipindi hiki cha maradhi,” alisema Mwananzila.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora alisema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu watu waliojitokeza kupima Ukimwi walikuwa ni 122,085, kati yao wanaume ni 57,763 na wanawake 64,322, ambapo watu 5,342 walikutwa na maambukizi.
Alisema kwamba kati ya hao wanaume ni 2,284 na wanawake ni 3,065 sawa na asilimia 4 ya watu wote walijitokeza kupima. Awali Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Fikiri Martine alisema maambukizi ya Ukimwi mkoani humo yameshuka kutoka asilimia 6.4 hadi kufikia asilimia 5.1 kutokana na tafiti tatu zilizofanyika mkoani hapa.
Aidha alisema katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu mama wajawazito 87,841 walipima maambukizi ya virusi vya Ukimwi kati yao akinamama 936 ambao ni sawa na asilimia 1 waligundulika kuwa na maambukizi.
Alisema baada ya kubainika hivyo walianzishiwa dawa za kufubaza virusi hivyo (ARVs), chini ya mpango mahsusi wa kuwaanzishia dawa hizo akinamama wote waliogundulika kuwa na VVU.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Chanzo;Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa