Home » » SOKO KUU ULANGA LAUNGUA

SOKO KUU ULANGA LAUNGUA

SOKO Kuu la Wilaya ya Ulanga, lililopo Mahenge, limewaka moto na kuteketeza vyakula na bidhaa mbalimbali zenye thamani kubwa ya fedha.

Taarifa ambazo Tanzania Daima, ilizipata jana kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo zilisema moto huo ulizuka alfajiri ya kuamkia jana katika chumba kimojawapo cha fundi na mfanyabiashara wa vifaa vya simu.

Raphael Hamandusi (39), mmoja wa wafanyabiashara ambao mali zao ziliteketea, alisema moto huo ulianzia katika chumba cha mfanyabiashara wa vifaa vya simu aliyejulikana kwa jina la Sadiq Bahati.

Alisema inawezekana chanzo cha moto huo kikawa ni hitilafu ya umeme iliyotokana na kuchaji simu, kazi ambayo mfanyabiashara huyo huifanya nyakati za mchana na usiku.

“Ukweli tukio hili limetutia hasara kubwa sana maana tuliwekeza kwenye bidhaa tulizokuwa tumezihifadhi katika soko hili tuukisubiri wateja, mimi mali zangu zilizoteketea ni zaidi ya shilingi milioni 5.8" alisema Raphael.

Alitaja baadhi ya mali hizo ni Ulezi magunia 20, Mahindi magunia 28 na mchele maguni 30 na kuddai kuwa amefaulu kuokoa kiasi kidogo za Ulezi na mahindi.

Mwenyekiti wa soko hilo Athumani Kusa, alisema moto huo unakadiriwa kuanza majira ya saa 8 usiku, alifika eneo la tukio majira ya saa 9: 30 alfajiri na kukuta moto umteketeza kibanda cha mfanyabishara huyo wa simu na kushika baadhi ya majengo ya soko kuu.

“Mimi nilifika majira ya saa 9:30 usiku nikakuta hiki kibanda kimeteketea chote na moto umehamia kwenye soko kuu,” alisema Kusa.

Athumani alisema soko hilo lililojengwa mwaka 1955 na inawezekana mfumo na mpango mbaya wa wafanyabiasahara hao umechangia kuungua kwa kiasi kikubwa kwa soko na bidhaa zilizokuwamo.

Naye Diwani wa kata ya Mahenge, Gregory Mlimani, alilithibitishia Tanzania Daima, kutokea kwa moto huo ulioteketeza mali mbalimbali ambazo mpaka sasa thamani yake haijajulikana.

Alisema uongozi wa soko kwa kushirikiana na serikali ya kata na Halamashauri ya wilaya hiyo wameanza tathmini kuhakiki ili kujua thamani ya mali iliyoteketea katika soko hilo.
 Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa