Wengine hoi kwa kipigo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda.
Tukio hilo lilitokea juzi sambamba na tukio la kuuawa kwa askari wawili wa kituo polisi cha Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani.
Aidha, Jeshi la Polisi limeungana na Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) kuwasaka watu waliovamia Kituo cha Polisi Ikwiriri wilayani
Rufiji Mkoa wa Pwani na kuwaua askari hao na kupora silaha mbalimbali
zikiwamo bunduki na risasi.
Katika tukio la Tabora, kijana huyo anadaiwa kufa wakati
akifukuzwa na askari hao wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora kwa
lengo la kutaka kumtia mbaroni kwa tuhuma za kushiriki mchezo wa
kamari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, akizungumza na
NIPASHE alisema tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu saa 10.30
jioni katika mtaa wa Kadinya kata ya Ng’ambo.
Kamanda Kaganda aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni PC Yohana na MW
Daniel Isonda na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitete kutokana na
kujeruhiwa kwa kipigo na wananchi.
Alisema wananchi walianza kuwashambulia askari hao walipotaka
kuwakamata vijana watatu waliokuwa wakicheza kamari kijiweni katika eneo
la Ng’ambo mjini Tabora.
Vijana hao baada ya kubaini wanataka kukamatwa na polisi walianza
kukimbia na bahati mbaya mmoja wao alitumbukia ndani ya dimbwi la maji
na kuzama.
Kaganda alisema kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Edwin Kefa
(19), baada ya kutumbukia katika dimbwi hilo, alishindwa kuogelea na
hivyo askari waliokuwa wakimfukuza walimuokoa akiwa katika hali mbaya na
kukimbizwa katika Hospitali ya Kitete, lakini alifariki wakati
akipatiwa matibabu.
Alisema pamoja na askari hao kushambuliwa, Jeshi hilo litaendelea
kufanya msako mkali ili kuvunja vijiwe vyote vya wacheza kamari, wavuta
bangi na wanaotumia dawa za kulevya mkoani Tabora.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wananchi walichukua
uamuzi wa kuwashambulia askari hao baada ya kuona wakimpiga kijana
aliyepoteza maisha kabla ya kufikwa na mauti.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kitete, Dk. Yusuph Bwire,
alisema hali za askari hao zinaendelea vizuri na kwamba Isonda
alijeruhiwa begani na kichwani.
Dk. Bwire alisema Yohana alijeruhiwa kichwani na kwamba aliruhisiwa jana asubuhi baada ya hali yake kuwa nzuri.
JWTZ YAJITIOSA RUFIJI
Wakati hayo yakitokea, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu
waliokiteka na kukivamia kituo cha polisi Ikwiriri na kuwaua askari
wawili na kuiba silaha.
Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul
Chagonja, akizungumza katika mahojiano na Redio One katika kipindi cha
Kumepambazuka, alisema wanashirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) ili kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanatiwa mbaroni.
Kamishna Chagonja alisema hadi kufikia jana jioni hakuna mtu
aliyekuwa amekamatwa na wamebaini kuwa bomu lililorushwa katika kituo
hicho halikuwa moja bali yalikuwa mengi.
“Uvamizi ulikuwa mkubwa na inaonekana waliofanya tukio hilo
walikuwa si chini ya 15 na baada ya kufanya tukio hilo waliondoka kwa
kutumia Noah,” alisema.
Alisema mabaki ya bomu lililorushwa yamepekwa kwa wataalam kubaini ni bomu la aina gani.
Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, alisema tukio la kuvamiwa kituo hicho lilitokea saa 8:00 usiku.
Kamanda Matei alitaja askari waliouawa kuwa ni PC Judith Timoth na
Koplo Edga Mlinga ambaye ni askari wa kikosi cha usalama barabarani na
kwamba miili ya askari imehifadhiwa katika kituo cha afya Ikwiriri.
Alisema baada ya kukivamia kituo hicho waliiba bunduki aina ya SMG
mbili, SAR mbili, Shotgun moja, risasi zaidi ya 60 na bunduki mbili za
kulipulia mabomu ya machozi.
Matei alisema baadaye walilipua bomu kituoni hapo ambalo
liliharibu gari lenye namba PT 1965 linalotumiwa na Mkuu wa Upelelezi wa
Kituo hicho (OCCID) kisha kutokomea kusikojulikana.
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alisema jeshi hilo lina idara
nyingi, hivyo taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kushirikiana
katika uchunguzi wa tukio hilo zinaweza kuwa za kweli.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KUELEKEA UCHAGUZI 2015: JE UNAPENDA NANI AWE KIONGOZI WAKO? JAZA FOMU HII FUPI HAPA
docs.google.com
docs.google.com
0 comments:
Post a Comment