Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ZAIDI ya wanachama 130 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Manispaa ya Tabora,
wamefunga ofisi ya Katibu wa chama hicho Wilaya ya Tabora Mjini, Bw. Bakari
Lwasa na kuandamana hadi Ofisi ya CCM Mkoa ili kushinikiza aondolewe mara moja.
Wakiwa katika Ofisi ya CCM mkoani humo, wanachama hao walimkuta katibu wa chama
hicho mkoani humo, Bi. Janeth Kayanda, wakiwa na mabango yaliyokuwa yakimtuhumu
Bw. Lwasa kwa makosa ya ufujaji wa sh. milioni nane.
Baadhi ya mabango hayo yalisema; "Bakari hatukutaki, nenda kwenu Kaliua,
umekuja kuua chama, umeharibu chama chetu".
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, Bw. Deus Malugu alisema Bw. Lwasa
amekigawa chama hicho kwa muda mrefu, kushiriki njama za kuwachafua baadhi ya
viongozi na kushiriki kukikosesha ushindi CCM katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwaka 2014.
Alisema Katibu huyo ameshiriki katika upotevu wa sh. milioni nane za chama,
Kata ya Gongoni na kuanzisha matawi mawili ya CCM ambayo ni Mdoe na Bachu bila
kuwashirikisha wenzake jambo ambalo ni tabia ya ubinafsi.
Tuhuma nyingine zilizotolewa dhidi ya Bw. Lwasa ni kugawa sh.50,000 kwa
Makatibu Kata wawili (majina yanahifadhiwa), ili wawe mashahidi dhidi ya Mjumbe
wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Emmanuel Mwakasaka anayedaiwa kuanza kampeni ya
kutaka ubunge wa Jimbo la Tabora Mjini kabla ya muda.
Bw. Malugu alisema mgogoro baina yao na Bw. Lwasa upo muda mrefu ambapo
Mwenyekiti wa CCM mkoani humo ambaye amemaliza muda wake, Hassan Wakasuvi na
Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Bw. Abdulrahman Kinana, waliahidi kuupatia
ufumbuzi lakini hadi sasa wapo kimya.
Kwa upande wake, Bw. Lwasa alipoulizwa juu ya tuhuma hizo, alisema yeye hajui
lolote na hafahamu kama wanachama hawamtaki au kuna maandamano ya kumkataa.
"Mimi sijui kama hawanitaki, sijui kama kuna wajumbe ambao wameandamana
kwenda Ofisi ya Katibu wa CCM Mkoa kunikataa na sina taarifa kama ofisi yangu
imefungwa," alisema.
Baada ya kupokea maandamano ya wanachama hao, Kayanda alipokea taarifa yao na
kuahidi kuyafanyia kazi malalamiko yao kwa kuyafikisha katika uongozi wa CCM
Taifa kwa hatua zaidi.
Alisema CCM Mkoa itampa Bw. Lwasa ofisi ya muda wakati wakisubiri uamuzi wa
mwisho kutoka kwa uongozi wa juu
Chanzo Gazeti la Majira
0 comments:
Post a Comment