Home » » IFAHAMU WILAYA YA IGUNGA

IFAHAMU WILAYA YA IGUNGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Jiografia

Wilaya ya Igunga ipo sehemu ya Kaskazini Mashariki mwa Mkoa wa Tabora. Ina eneo la kilometa za mraba 6,912 sawa na asilimia 11 ya eneo lote la Mkoa wa Tabora na ipo kati ya latitudo 3o51" na 4o48" Kusini na longitudo 33o22" na 30o8" Mashariki. Wilaya inapakana na Wilaya ya Kishapu kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Iramba upande wa Mashariki, Wilaya ya Uyui upande wa Kusini na Wilaya ya Nzega upande wa Magharibi.
Wilaya imegawanyika katika maeneo ya misitu, vichaka, mbuga za malisho na maeneo ya Tambarare. Wilaya ina aina tofauti za udongo na mwinuko wa kati ya mita 1,080 na 1,100 juu ya usawa wa bahari.
Wilaya hii ni miongoni mwa Wilaya kame hapa nchini ikiwa na wastani wa mvua kati ya mm 500 hadi mm 700 kwa mwaka. Hali ya joto huwa kati ya nyuzi joto 20oC – vipindi vya baridi hadi nyuzi joto30oC vipindi vya joto.
Eneo la Kaskazini mwa Wilaya hii lina mwamba ambao hautunzi maji wakati wa kiangazi; hivyo kutokuwepo visima vya maji. Katika eneo hili kuna tatizo kubwa la maji kwa ajili ya matumizi ya watu na mifugo wakati wa kiangazi.

Utawala

Wilaya ina tarafa nne ambazo ni Igunga, Igurubi, Manonga na Simbo; na pia ina kata 26,Vijiji 93 na Vitongoji 637 na mji mdogo wa Igunga.. Aidha Halmashauri ya wilaya ina Madiwani 26 wa kuchaguliwa na Madiwani tisa wa viti maalum. Wilaya ya Igunga ina jimbo moja la uchaguzi.

Idadi ya Watu

Kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wilaya ina jumla ya watu 399,727 (wanaume 195,607 na wanawake 204,120). Wastani wa ongezeko la watu kwa mwaka ni 2.3%. Idadi ya kaya zote ni 62,427. Wastani wa watu kwa kaya ni 6.4.

Hali ya Uchumi na Maendeleo ya Wilaya

Uchumi wa Wilaya unategemea zaidi kilimo na ufugaji ambacho kinaajiri takriban asilimia 90 ya wakazi wote wa Wilaya hii. Kutoka katika kilimo mazao ya chakula na biashara huzalishwa. Serikali ya Wilaya husaidiana na Sekta Binafsi katika utoaji wa huduma za kijamii na za kiuchumi ili sekta nyingine ziweze kujiendesha.
Aidha, mapato ya ufugaji, uvuvi, na shughuli za viwandani ni ajira mbadala zinazochangia katika pato la wakazi wetu.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa