MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ametoa siku 14 kwa Mkuu wa
Wilaya ya Kaliua, Hadija Nyembo awe amewasilisha taarifa juu ya mauaji
ambayo yametajwa kukithiri kwa kueleza hatua zilizochukuliwa.
Alitoa agizo hilo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika
juzi mjini hapa baada Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, kumweleza kuwa wilaya
hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa mawili ambayo ni mauaji na
unyang'anyi wa kutumia silaha na kwamba yamekuwa yakijitokeza mara kwa
mara katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Mwanri alisema serikali haiwezi kuendelea kusikiliza taarifa za
mauaji ya watu wasio na hatia kila siku wakati nchi inaendeshwa kwa
taratibu na sheria zilizopo, na yeyote anayekwenda kinyume anapaswa
kuchukuliwa hatua mara moja.
“Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Mkuu wa Polisi wa Wilaya, haiwezekani
kila siku tusikilize vitendo vya mauaji tu hapa Kaliua, tunapaswa
kuchukua hatua za makusudi mara moja kukomesha vitendo hivyo,” alisema
na kuendelea: “Natoa siku 14, mniletee taarifa za wahusika wote wa
vitendo vya mauaji na hatua zilizochukuliwa dhidi yao.”
Aidha alimwagiza Nyembo kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri, Athuman Kihamia na wataalamu wake kuhakikisha wanaonesha
wananchi maeneo yanayofaa na yale yasiyofaa kuishi ili kupunguza
migogoro.
Awali Nyembo, alitaja maeneo tete yaliyokithiri kwa vitendo vya
uhalifu ni Ulyankulu, Usinge,Ufulaga, Mkuyuni, Mwaharaja, Mpandamlowoka
na maeneo mengine yenye mapori ya hifadhi yanayokaliwa na watu isivyo
halali.
Alitaja chanzo cha mauaji hayo kuwa ni imani za kishirikina, visasi,
kuwania urithi wa mifugo na mashamba na kujichukulia sheria mkononi,
huku wahusika wa mauaji hayo wakiwa ni wazee wanaodhaniwa kuwa
washirikina kutokana na umri wao au kuwa na macho mekundu, wezi wa
mifugo na wenye mali.
Kuhusu unyang'anyi wa kutumia silaha, Mkuu huyo wa Wilaya alifafanua
kuwa matukio mengi yako vijijini ambako watu wanakaa na fedha nyingi
majumbani mwao hususan wakulima na wafanyabiashara, kwa madhumuni ya
kununua mazao au mifugo.
Alitaja sababu za kuongezeka vitendo hivyo kuwa ni kutafuta utajiri
kwa njia za haraka na kuwaondoa wenye fedha ili wengine warithi. Alitaja
waathirika wakuu kuwa ni wafanyabiashara wa mifugo, mazao, bidhaa za
madukani na mara chache waendesha mabasi.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment