Imeandikwa na Raymond Mushumbusi,
WAKALA wa Ufundi na Umeme (Temesa) imewazuia wamiliki na waendeshaji
wa karakana teule zilizopewa mamlaka na wakala huo kutengeneza magari na
vifaa vya Serikali, kutofanya matengenezo ya magari na vifaa hivyo bila
kufuata utaratibu wa wakala.
Akizungumza katika kikao kati ya Temesa, wamiliki na waendeshaji wa
karakana teule, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Temesa, Manase Lekujan alisema,
karakana teule zinatakiwa kufuata taratibu husika kufanya matengenezo ya
magari na vifaa vya Serikali.
“Tumeitisha kikao hiki na wamiliki wa karakana teule tunazofanya nazo
kazi ili tukumbushane kuhusu kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na
taratibu zilizopo kwenye mikataba yetu.
Hii ni katika kuweka mpango mzuri wa kuwa na taarifa sahihi za
matengenezo ya magari na vifaa vya Serikali katika karakana zetu ili
kuondokana na changamoto zilizopo na kuongeza ufanisi wa kazi zetu,”
alisema Manase.
Akifafanua kuhusu Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2011, Mwanasheria wa
Temesa, Gratian Mali alisema, sheria inatoa nafasi kwa Wakala huo
kutafuta karakana binafsi kusaidia shughuli za matengenezo ya magari na
vifaa vya Serikali pale ambapo karakana za wakala zinakuwa na kazi
nyingi au kukosa baadhi ya vifaa kwa ajili ya matengenezo na kazi hizo
hutolewa kwa vibali maalumu kutoka Temesa.
Akizungumza baada ya kikao hicho, mmoja wa wamiliki wa karakana ya
Nduvin Auto Works, Masoud Msangi, alisema kikao kimekuwa cha mafanikio
kwani imefika wakati kwa karakana teule kutekeleza agizo la kutengeneza
magari na vifaa vya Serikali kwa kufuata sheria na taratibu na sio
kufanya shughuli zake kiholela.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment