Home » » MIAKA 25 YA VYAMA VINGI

MIAKA 25 YA VYAMA VINGI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Michael Eneza

  • Jini limerudi kwenye chupa, au Magufuli atashindwa?
WAKATI wa mjadala wa kuingia au kukataa kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1991, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, hayati Rashidi Mfaume Kawawa, alisema kuwa hatuna budi kuingia katika mfumo mpya kwani utii wa jadi kwa Chama Cha
Mapinduzi haupo tena miongoni mwa Watanzania walio wengi.


Rashidi Mfaume Kawawa.
Alitumia nahau ya utamaduni wa Kiswahili kusema “jini limetoka kwenye chupa, huwezi kulirudisha,’ akichukulia utii wa watu kama kitu kikubwa, kikishabadilika mandhari yake, mwelekeo wake, basi.
Ni wazi kuwa awamu ya tano haijikiti katika hisia hiyo, ila ya utii kwa chama tawala, sivyo?
Mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani kwa awamu ya tano, ni wazi kuwa hakuna mfumo wa vyama vingi unaoendelea bali ule wa chama kimoja, kwani hali hiyo inaonekana kuwa ndiyo inayofaa kuleta nidhamu serikalini, na kurahisisha kupitisha maamuzi.
Eneo lake la kwanza ni kuzuia wabunge kuwasiliana moja kwa moja na wananchi kupitia vyama vyao vya siasa, ila kama wanafanya kazi walizopangiwa na dola, yaani kusimamia miradi ya maendeleo, na kujadili hayo tu.
Mengine zaidi ya hapo, yanayotokana na ajenda za upinzani, yanafuatiliwa kwa karibu kama hisia za uchochezi.
Swali linakuja kama hali hii ni kielelezo cha jinsi jamii ilivyosimama na kuridhia kurudi katika mfumo wa chama kimoja, kwani hata wakati ule wapo wengi tu ambao hawakuwa na imani na mfumo wa vyama vingi.
Ikiwa mazingira hayo ya kisaikolojia ni sahihi, kuwa mfumo au mwelekeo wa dola hauna tatizo uwe ni wa chama kimoja au vyama vingi, itakuwa ni utamaduni wa Mtanzania ulikuwa haujabadilika, hivyo mfumo wa vyama vingi ungekuwa ni raha ya aina fulani, au ukimnukuu Mwalimu vibaya, ni ‘ulevi tu.’ Ndivyo alivyosema mwanamapinduzi wa Russia, Vladimir Lenin, kukataa vyama.
Kwa upande mwingine, zipo nadharia za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa jumla ambayo ni pamoja na mabadiliko ya mpangilio wa fikra za watu kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda mfumo wa vyama vingi.
Nyakati zile za awali jamii ilikuwa inafikiria kijumlajumla, kwa mfano hatari ya Tanganyika kutawaliwa na mabeberu n a viongozi wapenda mabadiliko (wapinga mifumo ya kikoloni na kibepari) kuuawa, nchi kupinduliwa.
Ni hisia hiyo iliyoainisha umuhimu wa kumuunga mkono Mwalimu kwa ajili ya uhai wa taifa, na siyo kwa sababu kitamaduni hatujui upinzani, kuheshimu wazee.
Ina maana kuwa kwa mfumo huo wa hisia, kuunga mkono serikali kama jambo la lazima kwa uhai wa taifa, hisia hizo ziliambatanana na kipindi halisi cha woga kuhusu hatma ya taifa,, ambayo kwa upande mwingine iliendana na uchanga wa taifa na nafasi maalum ya Mwalimu Nyerere katika hisia za Watanzania.
Pale ambapo vigezo vyote hivyo havipo, ni kwa mantiki gani ambapo awamu ya tano inarudisha nidhamu ya chama kimoja, iwe ni kosa kuongea na kujumuisha watu kiupinzani, na huku vyama siyo tu vimeandikishwa bali vina wawakilishi wengi tu bungeni? Iweje wabunge na hasa wa chama tawala wawe radhi kwa hali hiyo, wapitishe kanuni kutotangazwa ila kwa mbinde shughuli za Bunge?
Ukianza kutafakari ridhaa ya wabunge wa chama tawala kwa hali iliyopo unaanza kupata majibu kuhusu mifumo ya hisia na malengo au mikakati ya kisiasa ya kurudisha utawala wa chama kimoja, kupunguza upinzani kwa kiwango kinachoridhisha kufifisha sauti yake, Siyo tena hisia ya kitaifa ya hatari ya kuwepo migawanyiko kati yetu, kuwa baadhi wanaweza kununuliwa na ubeberu wakawa mawakala wa kuvuruga nchi, livyosema Nyerere wakati akitetea sheria ya kuweka watu kizuizini (Preventive Detention Act) ya mwaka 1962.
Alikuwa akifungua kampasi ya Mlimani ya Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki kwa upande wa Dar es Salaam, Aprili 1964, kwamba ilikuwa lazima kabisa.
Kwa vigezo hivyo, siyo rahisi kwa chama tawala kutumia fikra ya jumla kuhusu umoja wa nchi na hatari zinazoikabili kutetea kurudisha mfumo wa chama kimoja katika utendaji wa kila siku.
Na isitoshe, urudishaji huo hauwezi kufikia mahali ambapo chaguzi halisi za vyama vingi zinaondolewa kabisa au uchaguzi unafutwa endapo matokeo ni hasi kwa utawala, jambo ambalo limewezekana kwa sehemu ndogo ya nchi isiyojitegemea.
Ingekuwa ni dola ya Visiwani yenye jukumu la kulinda maamuzi hayo isingefanikiwa au ingehitaji machafuko kama Burundi, ambayo ina maana kuwa hali hiyo si rahisi Bara.
Kinachoonekana katika juhudi hizo ni kuwa kulikuwa na ulazima wa kurudisha nidhamu katika utendaji serikalini na mashirika ya kiserikali, na maeneo mengine ya maisha ya nchi kwa jumla, kwa mfano katika kampeni dhidi ya madawa ya kulevya, au viroba.
Ina maana kuwa chama tawala kinaona kuwa vizuizi vyote hivi ni lazima ili kunusuru hali ya mkanganyiko kuhusu uongozi na maadili kwa jumla, iliyofikisha chama tawala katika hatari ya kunyang’anywa dola na upinzani. Inaashiria hisia ya kujilinda, kwa kuhofu upinzani, na siyo mshikamano halisi wa kitaifa kutaka ‘demokrasia ya chama kimoja.’
Tatizo hapa ni mazingira ambako mwafaka huu wa kihisia ndani ya chama tawala, kutoa sehemu ya uhuru wake kwa ‘Leviathan,’ mtawala madhubuti, ili anyooashe mambo yao pale ambapo wameshindwa kuyaendesha vyema kidemokrasia, yataendelea kudumu.
Yako maeneo mawili ya kuridhia hali iliyopo kwa sasa, moja ikiwa ni ndani ya chama tawala na nyingine ikiwa ni ndani ya jamii kwa upana wake, kwa maana kuwa hata upinzani kwa kiwango fulani unazuiliwa katika mielekeo yake na inachojua kinatawala hisia za watu. Wanataka mabadiliko, na hivyo serikali iliyopo inapewa muda ili ifuzu.
Kwa upande wa chama tawala, hali hii ya ‘demokrasia ya chama kimoja’ inaweza kuendelea kwa kipindi chochote mradi tishio la upinzani bado lipo, au tuseme kuna mtazamio kuwa baada ya kipindi cha mpito imani ya wananchi itakuwa imerejeshwa tena kwa CCM.
Uhuru hautaashiria tena uwezekano wa kuondolewa chama tawala, lakini kuna upande wa pili, kuwa sehemu ya chama tawala inaanza kuona kuwa uhuru ndiyo jambo muhimu, na kama inahitaji upinzani uingie madarkani ili uhuru uhakikishwe, ni vyema.
Kwa njia hiyo, utawala uliopo kutegemea mshikamano chama tawala si rahisi.
    CHANZO GAZETI LA NIPASHE

    0 comments:

     
    Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
    Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
    Designed by Fredy Tony Njeje
    Proudly powered by Blogs za mikoa