Imeandikwa na Lucas Raphael, Igunga
MKAZI wa Mtaa wa Kamando katika Kata ya Igunga Mjini wilayani Igunga
mkoani Tabora, Masumbuko Stephano (39) amefariki dunia papo hapo baada
ya kuchomwa kisu na mkewe Christina Elias (30) kwa wivu wa mapenzi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kamando, Julius Kitundu alisema
mauaji hayo yamefanyika Novemba 6, mwaka huu saa 7:15 usiku katika Mtaa
wa Kamando. Kitundu alidai Stephano alichomwa kisu wakati akiwa kwa
hawara yake, Happiness William (28) mkazi wa Mtaa wa Kamando.
Alidai mke wa marehemu alimfuata mume wake baada ya kugundua yuko kwa
hawara yake, ambako alifika na kugonga mlango kisha kuingia ndani na
kumchoma kisu mumewe upande wa kushoto katika eneo la moyo kisha mumewe
kuanguka na kupoteza maisha.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Habilo
Mhagama alikiri kupokea mwili wa marehemu Stephano, saa nane usiku wa
Novemba 6. Dk Mhagama alisema uchunguzi wa awali unaonesha mtu huyo
alipoteza maisha kutokana na damu nyingi kuvuja kutokana na kisu
alichochomwa kwenye moyo.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya
Igunga wakisubiri ndugu kuuchukua. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alithibitisha kuuawa kwa Stephano,
na kuongeza kuwa baada ya polisi kupata taarifa, walifika eneo la tukio
na kumkamata mke wa marehemu akiwa na kisu chake.
Kamanda Mutafungwa alisema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi
na kuongeza kuwa upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa
mahakamani.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment