Imeandikwa na Lucas Raphael, Igunga
KIJANA muuza dawa za binadamu anayeishi Kijiji cha Mazira Kata ya
Goweko, Igunga,Tabora, Shamsi Almasi (26) anashikiliwa na Polisi kwa
tuhuma ya kusababisha kifo cha kichanga cha siku moja cha kike.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Grayston Mushi alithibitisha tukio
hilo kutokea Novemba 8, mwaka huu saa 9 alasiri Kijiji cha Mazira, Kata
ya Goweko. Alisema Maria Andrea, mjamzito anayeishi Kijiji cha Buhekela
alipopatwa na uchungu alienda kwa huyo kijana Almasi kuzalishwa lakini
bahati mbaya mtoto alitanguliza miguu kichwa kikabaki. Alisema kijana
huyo baada ya kuona ameshindwa kumzalisha mama huyo mjamzito, aliamua
kunyofoa kiwiliwili cha kichanga hicho na kuacha kichwa tumboni mwa
mama.
Hata hivyo, alipoona hali hiyo alimwambia mume wa Maria, John
Isanzule (37) ampeleke Hospitali ya Ndala kwa matibabu zaidi huku mama
huyo akiwa hana fahamu. Aidha, Kamanda Mushi alisema baada ya kukamatwa
na kuhojiwa na Polisi, iligundulika kijana huyo hana taaluma ya udaktari
au ukunga wala uuguzi na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Akizungumza kwa shida akiwa amelazwa wodi ya wazazi Hospitali ya
Misheni ya Ndala, Maria alisema kijana aliyemzalisha alishindwa ndio
maana alinyofoa kiwiliwili cha kichanga na kuacha kichwa. Kaimu Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Misheni Ndala, George Mgalega amekiri kumpokea
Maria akiwa hajitambui. “Ni kweli tulimpokea akiwa hajitambui na
tulimfanyia upasuaji na kufanikiwa kutoa kichwa cha kichanga na hali
yake inaendelea vizuri baada ya kupatiwa huduma zote zinazostahiki,”
alieleza.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment