Mustapha Kapalata, Nzega
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora, jana ilipokea ombi la upande wa walalamikaji la kumtaka Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli ili afike mahakamani hapo Juni 19, mwaka huu, kujibu tuhuma zinazomkabili.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa kusikiliza maelezo ya mashahidi kwenye kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM).
Shauri hilo lilifunguliwa na mlalamikaji, Joseph Kashindye, aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA dhidi ya Dk. Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na msimamizi wa uchaguzi.
Mapema, Wakili Kayaga Kamaliza anayewakilisha upande wa Dk. Kafumu aliiomba mahakama hiyo itoe hati ya kumtaka Waziri Magufuli afike mahakamani hapo kupitia Ofisi za Bunge Dodoma.
Dk. Magufuli ni mmoja kati ya mashahidi muhimu wanaotegemewa katika kesi hiyo kwa upande wa utetezi.
Wakati akitoa maombi hayo, pande zote mbili za walalamikaji na serikali, hazikuwa na hoja za kupinga kufuatia wito huo kwa Waziri Magufuli.
Tuhuma zinazomkabili Magufuli ni pamoja na kutoa ahadi za ujenzi wa daraja la Mbuntu ambalo ni moja ya changamoto jimboni humo, kutao ahadi za kugawa mahindi ya njaa kwa wananchi wa jimbo hilo, na viapo kwa baadhi ya ahadi alizokuwa akizitoa katika majukwaa ya kumnadi Kafumu kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga.
Jaji Mery Shangali, akitoa uamuzi juu ya hati hiyo alisema kuwa, mahakama imekubali ombi hilo la kuituma kwa Waziri Magufuli ili afike mahakamani hapo tarehe hiyo kutoa ushahidi wake.
Wakati huo huo, Profesa Abdallah Safari anayemtetea Kashindye, aliiomba mahakama hiyo iahirishe shauri hilo kufuatia mazishi ya muasisi wa CHADEMA, Bob Makani, yaliyofanyika jana mkoani Shinyanga, akidai ni lazima naye ahudhurie kama mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho.
Jaji Shangali alikubali, na hivyo kuihairisha kesi hiyo hadi leo ambapo itaendelea kusikilizwa, huku mashahidi zaidi ya 43 wakiwa wametoa ushahidi wao, 20 wakiwa ni upande wa mlalamikaji na 20 kwa upande wa utetezi pamoja na Magufuli na washtakiwa wengine wawili.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment