Home » » DIWANI IGUNGA ADAIWA KUTAFUNA MICHANGO YA WANANCHI

DIWANI IGUNGA ADAIWA KUTAFUNA MICHANGO YA WANANCHI

Na Abdallah Amiri, Igunga
DIWANI wa Kata ya Kining’inila wilayani Igunga, mkoani Tabora, Raphael Ngassa (CCM), anadaiwa kula michango ya wananchi iliyochangwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kining’inila.

Upotevu wa fedha hizo zinazokadiriwa kufikia Sh 2,132,600 na mifuko 137 ya saruji, zilibainishwa baada ya Mtendaji wa Kijiji hicho, Abeli Isaka, kusoma taarifa ya mapato na matumizi kijijini hapo mwishoni mwa wiki.

Awali, Isaka aliwaambia wananchi hao kuwa hawezi kusoma mapato na matumizi kwa kuwa tangu aripoti kijijini hapo mwaka 2010, hajawahi kukabidhiwa ofisi na mali zilizopo licha ya kuomba bila mafanikio.

Hata hivyo, wananchi walimlazimisha awasomee chochote kilichopo na aliposoma taarifa hiyo, wananchi walipigwa na butwaa kusikia kwamba taarifa ya kijiji hicho haijawahi kusomwa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita na vitabu vyote vinavyoonyesha orodha na michango ya wananchi katika kipindi hicho, havijakabidhiwa kwa mtendaji huyo na diwani wao aliyekuwa anashikilia wadhifa huo.

“Uongozi uliopita wa kata, kijiji kwa usimamizi wa diwani, umeshindwa kukabidhi vitabu na nyaraka zote za ofisi jambo lililosababisha kazi za maendeleo kuwa ngumu.

“Hata hivi leo, siwezi kusoma mapato na matumizi pamoja na michango mingine ya vyumba vya madarasa na nyumba za walimu kwa sababu sina vitendea kazi zikiwamo nyaraka nyingine, ladba diwani wenu ambaye alikuwa anashikilia nyadhifa zote hizi, aje awasomee taarifa hiyo,” alisema Isaka.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mtendaji Kata ya Kining’inila, John Salamba, amekiri kuwapo kwa malalamiko ya wananchi kutosomewa mapato na matumizi katika kipindi cha miaka minne.

Aidha, alisikitishwa na hatua ya diwani kuficha vitabu na stakabadhi za mapato na matumizi, akisema hatua hiyo hailengi kuonyesha utawala bora na kumtaka diwani huyo kuheshimu mawazo ya wananchi kwa kuvirudisha mara moja katika ofisi ya kijiji.

Alipoulizwa, kuhusu madai hayo, Diwani Iduta, alikiri kufahamu michango ya wananchi lakini alisema baadhi ya mifuko ya saruji iliharibika hivyo inahitajika kununuliwa mingine na kuhusu fedha hatambui madai hayo.

Kutokana na mtafaruku huo, wenyeviti watatu wa vitongoji, majina yao katika mabano wa CCM, wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Madiwani hao ni Mchani Mazitiya (Luyeye Madukani), Changu Saguda (Masanga Mashariki) na Temagila Lushinge (Isera Madilu).
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa