na Mwandishi wetu, Igunga
HOSPITALI ya Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora imepokea msaada wa vitanda 28 vya kisasa kwa ajili ya wodi ya wazazi na wagonjwa mahututi, na vifaa vingine vyenye thamani ya zaidi ya sh milioni 400 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Igunga, Dk. Peter Kafumu (CCM).
Mbunge huyo pia aliikabidhi hospitali hiyo vifaa vya upasuaji, viti vya kusaidia wagonjwa, magodogo matano pamoja na sare za wahudumu na madaktari.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Joseph Kisala, alipokuwa akizungumzia changamoto zinazoikabili hospitali hiyo ya wilaya.
Dk. Kisala alisema pamoja na kuwapo kwa changamoto za upungufu wa watumishi hospitalini hapo, lakini misaada ya hali na mali inayotolewa na wadau imeendelea kuwahamasisha kufanya kazi kwa moyo.
“Kwa kweli Mbunge wetu Dk. Kafumu ametusaidia sana, alipochaguliwa tu alianza kupita na kuangalia mahitaji ya idara hii, na sasa ameweza kutimiza ahadi hiyo kama alivyokuwa amesema,” alisema Dk. Kisala.
Alisema kuwa msaada wa vitanda vya kisasa uliotolewa na mbunge huyo umeelekezwa katika wodi za wazazi na ile ya kupumzika baada ya kujifungua, wagonjwa mahututi na watoto.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema na kuonesha furaha zao wakisema kuwa msaada umewafikia katika wakati muafaka, huku wengine wakidaiwa kujimwaga mitaani kusherehekea.
“Tumeshukuru kuona kwa muda mfupi mbunge ameonyesha mapenzi makubwa kwa wapiga kura wake kwa kuanzia hospitalini, lakini pia sisi wananchi tunadhani tulichelewa kumpata huyu, leo Igunga ingekuwa mbali kimaendeleo,” alisema Jumanne Kizugwe mkazi wa Kijiji cha Mbutu.
Akizungumzia maradhi yanayoikabili jamii kwa sasa, Dk. Kisala alisema ugonjwa wa malaria umekuwa tishio kwa wananchi wilayani humo, ukifuatiwa na maradhi ya maambukizi na kuhara na kuhara damu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment