Home » » POLISI WAUA MAJAMBAZI WANNE

POLISI WAUA MAJAMBAZI WANNE

Na Frank Geofray, Jeshi la Polisi, Tabora
WATU wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wameuawa mkoani Tabora wakati wa mapambano makali ya kurushiana risasi baina yao na polisi. Tukio hilo lilitokea baada ya watu hao kufanya jaribio la kuvamia eneo la Congres Centre, huku wakiwa wamefunika nyuso zao kwa vitambaa vyeusi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora, Antony Rutta, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 25, mwaka huu saa 9 mchana katika Kijiji cha Kaliua Magharibi.

“Watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wameuawa katika mapambano makali ambayo yalikuwa ni ya kurushiana risasi.

“Wakati wa tukio hilo, vijana wetu walifanikiwa kuwadhibiti majambazi hao kwa sababu bunduki walizokuwa wakitumia hazikuwa kubwa,” alisema Kamanda Rutta.

Alisema eneo walikouawa majambazi hao, ni maarufu na hutumiwa na wafanyabiashara wengi wanaotoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Alisema majambazi hao, walikuwa wakitumia bunduki aina ya Shot Gun, iliyokuwa na risasi 12 na maganda sita ya risasi yaliokotwa.

“Baada ya mapambano makali, watu hao walipigwa risasi wote, tulipowachunguza tulikuta maganda sita ya risasi za Shot Gun ambazo zilirushwa,”alisema Kamanda Rutta.
.
Baada ya watu hao kutolewa vitambaa usoni, alisema jambazi mmoja aliyeuawa, alitambulika kwa jina la Masud Haruna, mkazi wa Kijiji cha Imalamihayo wakati wengine bado hawajatambulika.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu ili kuhakikisha wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Chanzo: Mtanzania

1 comments:

Anonymous said...

HI

Asante kwa Blog Ushauri tunataka picha zaidi maelezo bila picha yanachosha

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa