Home » » Baraza la Maadili lawaweka kitimoto vigogo kwa tuhuma mbalimbali

Baraza la Maadili lawaweka kitimoto vigogo kwa tuhuma mbalimbali

Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli
 
Baraza la Maadili ya Utumishi wa Umma limeanza kikao cha tatu cha kusikiliza malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma.
Wakati wa kikao hicho mashauri ya watuhumiwa tisa yatasikilizwa, kati yao watano wakituhumiwa kufanya matumizi mabaya ya madaraka na wanne ya kushindwa kuwasilisha matamko ya rasilimali zao.

Kikao hicho kinachofanyika mjini Tabora, kitachochukua takribani siku kumi, na kina washirikisha Mwenyekiti wa Baraza la Maadili, Balozi Hamis Msumi na wajumbe wawili wa baraza hilo, Hilda Gondwe na Celina Wambura.

Akizungumzia kikao hicho, Kamishna wa Maadili, Jaji Salome Kaganda, alisema ni cha kwanza kusikiliza malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi tangu baraza hilo lilipoteuliwa na kuapishwa Julai 11 mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.

“Kwa kuzingatia madhumini ya baraza na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika jamii, viongozi wamekuwa wakituhumiwa kuuza dawa za kulevya, kuhujumu mali za umma na kujilimbikizia mali jambo ambalo linaondoa imani kwa jamii hivyo ifikie wakati hatua zichukuliwe dhidi yao” Alisema Jaji Kaganda.

 Amewataka viongozi kuanzia ngazi za juu za maamuzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili kazini kwani sheria haitaangalia nafasi ya mtu au cheo chake kwa lengo la kulinda rasilimali za nchi.

Viongozi watakaofikishwa na Sekretarieti ya Maadili katika Baraza la Maadili ya Utumishi wa Umma ni, Mbunge wa Rorya, Lameck Airo, Diwani wa Kata ya Kanazi Wilayani Ngara, Mathias Mgata Bisoma na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Casmir Sumba Kyuki.

Wengine ni, Mkurugenzi Msaidizi Uandishi wa Sheria, Sarah Kinyamfura Barahomoka, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Spora Liana, Hakimu Mkazi Mfawidhi Sengerema, Liveta Msangi, Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Henry Matata, Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli na Suleiman Suleiman.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa