Home » » MAKALA-SERIKALI ITUWEKEE MAZINGIRA WEZESHI WAJASILIAMALI WADOGO TUTAFANIKIWA.‏

MAKALA-SERIKALI ITUWEKEE MAZINGIRA WEZESHI WAJASILIAMALI WADOGO TUTAFANIKIWA.‏


  Mjasiliamali Immaculata Kadidi akiwa kazini kwake

 Na Hastin Liumba,Tabora
SERIKALI ikiweka mazingira wezeshi kwa wajasiliamali wa chini tutapiga
hatua kubwa kimaendeleo na kukuza mitaji yetu kiisi cha kufikia hatua
ya kukopesheka.

Kauli hiyo ni ya mjasiliamali Immaculata Kadidi ambaye ni fundi
cherehani anayefanya shughuli zake katika kata ya Kanyenye barabara ya
Kitunda katika manispaa ya Tabora.

Kadidi alifanya mahojiano na mwandishi wa makala hii na kusema yeye ni
mjasiliamali wa kiwango cha chini hivyo anaamini kuwa serikali
ikiwakumbuka wajasiliamali wadogo itafikia hatua kwao kuaminika kwenye
mikopo katika taasisi za kibenki.

Anasema akiwa mjasiliamali kama fundi cherehani alianza kazi hiyo
mwaka 2004 hadi sasa na kwamba amekuwa akiendesha maisha ya familia
yake yenye watoto watano kwa kutegemea kazi za ufundi cherehani.

Kadidi alisema bado wajasiliamali wa chini na kati hawana elimu ya
kutosha kufanya kazi zao kwa ufasaha na ifikie mahali sasa serikali
ilione hilo sanjari na kuweka mazingira wezeshi ili kundi hilo ambalo
ndilo kubwa liingie kwenye ukombozi wa kweli.

Anasema amekuwa akipata wakati mgumu sana kuweza kupata mtaji hasa
mkopo toka taasisi kubwa za kibenki kiasi cha kufikia mahali kuona
kuwa serikali imelitupa kundi hilo ambalo likiwekewa mazingira huru na
sahihi ni dhahiri taifa litakuwa na kuendelea.

“Licha ya kukosa mkopo wenye tija kwangu bado nimekuwa nikihudumia
familia yenye watoto watano wanaosoma shule kwa kazi yangu yangu hii
ya ufundi wa cherehani.” alisema.

Anafafanua kuwa maisha anayoishi na familia yake mahitaji yote muhimu
katika maisha nategemea ufundi wa nguo hivyo bado anaona hatua
aliyopiga anastahili kusogea mbele zaidi.
Kazi zake.

Kadidi anasema ufundi wake wa nguo za kiume na kike amekuwa akitegemea
kununua vitambaa vya nguo katika mikoa ya Dar-es-Salaam na Mwanza na
licha ya ushonaji bado amekuwa akiuza na vitambaa katika duka lake.

“Hadi sasa toka nimeanza kazi ya ushonaji cherehani nimefanikiwa
kununua vichwa vya cherehani vitatu ambavyo ni vya kushona,kudarizi na
kukamilishia nguo na zote ni nzima zinafanya kazi.”alisema Kadidi.

Hata hivyo anasema biashara yake ya ushonaji bado ina tatizo moja
ambalo ni biashara ya msimu kwani kipindi cha kiangazi mara nyingi
biashara inakuwa ngumu hasa kwa kuwa hakuna sikukuu nyingi.

Anasema amekuwa akifanya biashara kipindi cha mwezi wa disemba na
januari kutokana na miezi hiyo kuwa kwenye sikukuu za Kristmas,mwaka
mpya na hata Pasaka.

Anaongeza miezi hiyo kama umechukua mkopo unaweza rejesha bila tatizo
lakini baada ya muda huo kupita ni tatizo kubwa kwani miezi mingine
biashara inakuwa ngumu kwani wateja wanakuwa wachache.

Alisema analazimika kutumia njia mbadala ili aweze kuendesha maisha
yake kwa kufanya biashara ya duka na kuuza vyakula, vitambaa,
stifu,vifungo,nyuzi,zipu na mafuta ya vyerehani na vitu vinginevyo.

Kuhusu mitaji na ugumu wa kazi zake.

Kadidi anaongeza kuwa kuhusu upatikanaji mitaji kwake ama
wajasiliamali wengi kama yeye bado ni tatizo kwani kazi za ufundi wa
chereheani inaonekana kama kipato chake ni kidogo sana kiasi cha
kufikiria endapo atakopa benki na kupata mkopo atarejeshaje.

Alisisitiza zaidi kuwa mafundi wote wa nguo wamekuwa wakiishi maisha
ya kawaida yasiyo kuwa na upigaji hatua wala kuwa na tija kwa kukosa
mitaji ama mikopo mikubwa.

“Leo hii unaweza kwenda benki kukopa kama nilivyojaribu kipindi fulani
pale CRDB benki niliomba mkopo wa milioni moja nikaambiwa mkopo ni
kuanzia sh milioni tano huku nikiulizwa nina mali isiyohamishika.

Anasema anatamani siku moja anaweza kufanikiwa kupata mkopo mkuwa wa
zaidi ya million moja na ataweza kufanya kiti kinachoeleweka kwa
kungua ofisi yenye vifaa vya kiasasa zaidi na hapo ndoto yake itakuwa
imetimia.

Alisema hapo alipo hana nyumba wala kitu kisichohamishika na hapo ndio
tunaona ipo haja serikali ikaliona hilo na kulifanyia kazi ili
wajasiliamali kama sisi tunufaike.

Alisema licha ya hayo bado hata mkopo wenyewe mlolongo wake unakuwa
mkubwa sana tofauti na wenzetu wenye mitaji mikubwa.

Aidha Kadidi anasema unaweza ukajaza fomu za kuomba mkopo huku
biashara yake inategemea msimu wa mwezi disemba hadi januari lakini
mkopo unaweza ukaupata mwezi machi na kipindi hicho wateja wa kushona
nguo wanapungua hapo ndipo baadhi ya wakopaji hukimbia deni.

Changamoto kubwa kwa wajasiliamali.

Kuhusu iliyoko mbele yake na wajasiliamali wengine wa chini ni elimu
kwani wamekuwa wakifanya kazi zao bila kuwa na elimu ambayo
ingewasaidia kufikia malengo yake.

Alisema hapo ndipo serikali inabidi kuweka mazingira kwao ya kuwapatia
elimu ya namna ya kufanya kazi za kijasiliamali.

Kadidi alisema na imani kubwa hata yale mabilioni ya rais Dk Jakaya
Kikwete hayakufikiwa malengo yake kutokana na wakopaji kukosa elimu ya
ujasiliamali.

Alisema amefanya utafiti kuwa hata wale wafanyabiashara wakubwa hawana
elimu ya biashara na walio wengi wamekuwa wakifanya kazi ama biashara
zao kwa uzoefu tu na si vinginevyo na mara nyingine wengi
wanafilisika.

Alisema anatoa wito na ushauri kwa serikali kutilia mkazo suala la
elimu kwa wajasiliamali wa chini na kuweka mazingira wezeshi na hilo
likifanyika taifa hili kupitia sekta  ya viwanda vidogo litakuwa kwa
kasi na uchumi utaimarika.

Anaongeza kuwa endapo elimu itatolewa kwa ufasaha kwa wajasiliamali
suala la kuzalisha bidhaa zenye ubora kama serikali inavyotaka hata
masoko ya ndani na nje hayatakuwa na tatizo kwao.

Kadidi anasema ujuzi wake aliipata jijini Dar-es-Salaam akiwa na
kikundi cha watu zaidi ya watano kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni
mwaka 1993.

NA Tabora yetu blog
www.tabora-yetu.blogspot.com

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa