Home » » Meya Tabora hatarini kung’olewa

Meya Tabora hatarini kung’olewa

SAKATA la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kutaka kumng’oa kwa mara nyingine Mstahiki Meya Ghulam Dewji Remtullah, limeibuka upya.
Awali meya huyo alinusurika kung’olewa mara tatu baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tabora kuingilia kati na kumnusuru.
Aidha kwa mara nyingine juzi madiwani hao wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa maalumu walitaka kumng’oa, lakini serikali ya mkoa iliingilia kati ikitaka kanuni zifuatwe.
Katika kikao cha juzi, madiwani hao walikuja juu kwa madai kuwa tuhuma za meya huyo ni kubwa na lazima awajibike.
Safari hii ni kama uongozi wa chama mkoa, wilaya na serikali wamejivua kwenye sakata hilo ambapo karibu madiwani wote wamemkataa.
Novemba 19 mwaka huu, kamati ya madiwani wa CCM waliitisha kikao cha dharura ili kujadili tuhuma zake ambapo madiwani waliohudhuria walikuwa 34 na kati yao 32 walimkataa.
Baadhi ya madiwani waliohudhuria kikao hicho waliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamemkataa meya huyo na kumtaka apime tuhuma zake na ajiuzulu yeye mwenyewe kabla hawajaamua kumng’oa.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa