Wengine wanne walifanikiwa kutoroka baada ya kukurupushwa wakati wakiteka magari Barabara ya Mwanza-Dar es Salaam.
Nzega. Jeshi la Polisi wilayani Nzega limempiga risasi na kumuua jambazi mmoja kati ya watano baada ya kuwakurupusha walipokuwa katika harakati za kuteka magari Barabara Kuu Mwanza- Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Peter Ouma
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo saa sita usiku katika Kijiji cha
Undomo, ambapo alisema majambazi hao tayari walishateka magari kadhaa.
Ouma alisema majambazi hao wakiwa na silaha za jadi, waliyateka magari kadhaa na kuwapa kipigo waliokuwa ndani.
Ouma alisema polisi walipata taarifa za kuwepo
majambazi hao baada ya dereva mmoja kukwepa mtego wa mawe yaliyowekwa
barabarani na kisha kuwafahamisha.
Dereva huyo baada ya kufika sehemu waliyojificha
majambazi hao aliona mawe yamepangwa barabarani ili kuzuia magari
yasipite, huku pia magari mengine kadhaa yakiwa yametekwa na majambazi
hao waliokuwa na mapanga, visu na marungu.
“Baada ya kuona mtego huo, dereva huyo alifanikiwa
kuruka mawe hayo na kupita bila madhara na kwenda kutoa taarifa
polisi,” alisema Kamanda Uoma.
Baada ya kupokea taarifa polisi walifika mara moja
eneo la tukio na kuanza kuwashambulia majambazi hao na mmoja kupigwa
risasi na kufariki dunia, huku wengine wakikimbilia porini.
“Jambazi mmoja alipigwa risasi na kufariki papo
hapo, na wengine baada ya kuona mwenzao ameanguka chini walitimua mbio
kwenda kusikojulikana,” alisema zaidi Kamanda Ouma. Kamanda Ouma
alimtaja jambazi aliyeuawa kuwa ni James Makoli (22) mkazi wa Gongo la
Mboto, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ouma, mpaka tukio hilo linatokea,
magari kadhaa yalishatekwa na majambazi hao, zikiwemo Toyota Land
Cruiser nne . Aidha, majambazi waliofanikiwa kutoroka walishapora kiasi
cha Sh600,000 kutoka kwa watu waliokuwa kwenye magari waliyoyateka.
Upelelezi wa awali unaonyesha kuwa majambazi hao
hutoka Dar es Salaam kwa kushirikiana na wale kutoka Mwanza. Ouma
aliwataka madereva wa magari kuongeza ushirikiano na polisi kwa kutoa
taarifa haraka wanapokutana na matatizo barabarani na pia kuepuka
kusafiri usiku.
Chanzo;Mwanaanchi
Chanzo;Mwanaanchi
0 comments:
Post a Comment