Home » » TAMASHA LA ‘ROSE MHANDO’ VURUGU TUPU, LAVUNJIKA.

TAMASHA LA ‘ROSE MHANDO’ VURUGU TUPU, LAVUNJIKA.


-RC na DC waondoka kwa huzuni.
 
Na Hastin Liumba, Tabora
 
TAMASHA la muziki wa injili lililokuwa lifanyike mjini Tabora
liligeuka kuwa uwanja wa sarakasi baada ya mashabiki waliofurika
katika uwanja huo kuanzisha vurugu baada ya kutomwona Rose Mhando
aliyekuwa akisubiriwa.
 
Hali hiyo ilianza baada ya mashabiki lukuki kujazana katika jukwa kuu
la uwanja huo wakimsubiri kwa hamu kubwa mwanamuziki huyo nguli wa
muziki wa injili hapa nchini  lakini kwa mshangao mkubwa hakuonekana
na hakuna kiongozi yeyote aliyeweza kutoa taarifa sahihi juu ya ujio
wake.
 
Mashabiki hao ambao walianza kuingia uwanjani hapo toka saa 4 asubuhi
ili kuwahi nafasi ya kumshuhudia mkali huyo wa injili, walishikwa na
bumbuwazi baada ya kutoonekana kwa mgeni huyo licha ya matangazo
lukuki ya ujio wake ya wiki nzima katika radio, mabango na magari.
 
Mbona hatumwoni Rose? Amekaa wapi? Mbona MC hatangazi kama yupo au
hayupo uwanjani? Sisi tumelipa hela kuja kumwona Rose hizi kwaya
zingine tumezizoea, kama hajafika watatutambua, hatukubali labda
waturudishie 2000 na 5000 zetu, alisema kwa jazba Katarina Peter.
 
Hawa jamaa wametutapeli haiwezekani utangaze wiki nzima kwamba Rose
Mhando anakuja halafu asionekane, huu ni wizi warudishe hela zetu,
afadhali hela zetu tungetoa sadaka kanisani kuliko kuibiwa kiujanja
namna hii, wakatubu mbele za Mungu, alisema Joseph Ngerera.
 
 Baada ya kuona masaa yanazidi kuyoyoma na bado haonekani wananchi hao
walianza kupiga kelele za kutaka hela zao mbele ya Mgeni rasmi mkuu wa
mkoa wa Tabora Fatma Mwassa aliyeambatana na mkuu wa wilaya ya Tabora
Suleiman Kumchaya, hali ambayo ilileta sintofaham katika uwanja huo.
 
Licha ya MC kuruhusu kwaya ya wenyeji ‘Gospel Music Campain Band’
kutumbuiza, mashabiki walianza kuondoka kwa hasira, hivyo askari
polisi wakalazimika kuingia uwanjani ili kurejesha amani iliyoanza
kutoweka huku wakiruhusu msafara wa mgeni rasmi kuondoka uwanjani hapo
baada ya kuona hali si shwari.
 
Kiongozi wa bendi iliyokuwa inazindua nyimbo zake aliyemwalika Rose
Mhando, Egon Israel alisema kitendo cha mgeni wake kutotokea katika
tamasha hilo la muziki wa injili bila taarifa kimemsikitisha sana kwa
kuwa alishalipwa kitita cha sh milioni 2 taslimu na aliahidi kuwepo
siku hiyo ndio maana walitangaza sana.
 
Alisema maandalizi ya tamasha hilo yamegharimu zaidi ya sh milioni 3.5
na kuongeza kuwa badala ya wananchi kupata amani, furaha na shangwe
katika Bwana wameambulia vurugu na
makwazo katika mioyo yao baada ya Rose Mhando kutooenekana.  Hili
limeniuma sana ila namwachia Mungu.
 
Mama Eric na Pastory Papo wanakamati katika maandalizi ya tamasha hilo
walisema kuwa kutofika kwa Rose Mhando kumewaumiza sana kwa sababu
walikuwa wanawasiliana naye tokea mwanzo wa maandalizi hadi siku moja
kabla ya tamasha kufanyika, wakashangaa kwa nini hakutoa taarifa kama
alijua hatakuja.
 
Hii ni aibu tupu, tunaomba waimbaji wawe wa kweli, tumwogope Mungu,
Rose Mhando ametufedhehesha kwa kutokuwa muwazi, tungealika waimbaji
wengine kama akina Bahati Bukuku. Hata hivyo tutakaa kikao ili tujue
la kufanya, waliongeza.
 
Na Tabora yetu Blog 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa